
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS kupitia ofisi zake za Kanda ya Mashariki unajipanga kuongeza uzalishaji miche bora ya miti na kutoa elimu hio kwa jamii kwa kutoa mafunzo maalumu ya siku tano kwa watumishi wake mkoani Morogoro.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TFS Prof. Dos Santos Silayo jana Septemba 18, 2023 wakati akifungua mafunzo hayo, Kaimu Kamanda wa Kanda ya Mashariki Mathew Ntilicha alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo na weredi watumishi katika kuanzisha na kusimamia vitalu vya miche bora ya miti.

“Mafunzo haya ni sehemu ya mkakati wa TFS kuhakikisha tunaongeza uzalishaji wa miche bora ya miti kwa kuzingatia kalenda ya bustani! Sisi Kanda ya Mashariki katika kuhakikisha hilo linafanikiwa wasimamizi wetu wa bustani 14 leo wanapata mafunzo yatakayowawezesha kuongeza uzalishaji na kupanda aina za miti ambayo inaendana na mazingira ya maeneo waliopo,” anasema Kaimu Kamanda wa Kanda ya Mashariki.
Aidha aliwataka watumishi hao kuhakikisha pamoja na mambo mengine kuiwezesha jamii kupata elimu zaidi kuhusu utunzaji wa miti ili kuhakikisha wanachangia katika uhifadhi wa mazingira kwa weledi.

Mafunzo hayo ya siku tano yanafanyika katika kituo cha mbegu Morogoro kuanzia Septemba 18 hadi 22, 2023 yakijumuisha watumishi 14 kutoka Ofisi za TFS – Kilombero, Mvomero, Malinyi, Ulanga, Kilosa, Morogoro, Chalinze, Temeke, Mafia, Kisarawe, Rufiji na Kibiti.
Tarehe 27 Machi 2023 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango wakati akizundua kampeni ya kupanda miti kitaifa kwa hisani ya Benki ya NMB ikishirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Jijini Dodoma aliziagiza Halmashauri kwa kushirikiana na TFS, kupanda aina za miti ambayo inaendana na mazingira ya maeneo waliopo pamoja na kuiwezesha jamii hususani ya vijana kupata elimu zaidi kuhusu utunzaji wa miti ili kuhakikisha wanachangia katika uhifadhi wa mazingira kwa weledi.