MBUNGE MAVUNDE APANIA KUPAISHA UFAULU WA MASOMO YA SAYANSI,AGAWA VIFAA VYA MAABARA SHULE ZA SEKONDARI DODOMA JIJI

Mbunge wa Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde leo amegawa vifaa vya maabara kwa shule za sekondari Wella,Makutupora na Mtemi Chiloloma vyenye thamani ya Tsh 9,000,000 kwa lengo la kusaidia kuongeza maarifa kwa wanafunzi wa mchepuo wa masomo ya Sayansi.

Mavunde amegawa vifaa hivyo leo katika shule ya Sekondari Wella katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Madiwani na Mkurugenzi wa Jiji.

“Dhamira yangu kubwa ni kuendelea kuunga mkono juhudi za Mh Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha elimu.

Naamini vifaa hivi vya maabara vitaongeza maarifa zaidi kwa wanafunzi wetu kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi na hivyo kupelekea kuongeza ufaulu kwa masomo ya sayansi.

Hii ni awamu ya kwanza nimeanza na shule hizi,lakini nitaendelea kugawa vifaa hivi kuzifikia shule nyingi zaidi za Jiji la Dodoma.

Pia tutatumia uwepo wa mkongo wa Taifa wa mawasiliano kuongeza ufanisi katika kufundisha masomo ya sayansi”Alisema Mavunde

Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Ndg. John Lipesi Kayombo ameshukuru mchango mkubwa unaotolewa na Mbunge Mavunde kwenye sekta ya Elimu kuahidi kuunga mkono jitihada za Mbunge katika kuwainua wanafunzi katika ufaulu wa masomo ya sayansi.

Wakishukuru kwa pamoja,madiwani wa kata za Kikuyu Kusini Mh. Anselm Kutika na Mh. Gideon Nkana Diwani wa Kata ya Hombolo Makulu wamemshukuru Mbunge Mavunde kwa namna ambavyo anajitoa kuwahudumia wanadodoma kupitia sekta ya Elimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *