
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kuwa imeongeza kasi ya kuboresha miundombinu, makazi na huduma za jamii kwenye maeneo ya mijini na vijijini ili kuhakikisha kuwa watu wote wanaishi katika makazi bora na salama.
Hayo yamesemwa leo Jijini Nairobi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula , kwenye Mkutano wa Shirika la Makazi unaoendelea Jijini humo.
Akitoa tamko la nchi kwenye Mkutano Mkuu wa Shirika la Makazi Duniani ulioanza jana Jijini Nairobi, ambao kauli mbiu yake ni “hatma ya miji endelevu kupitia ushirikishwaji na uwepo wa mifumo ya mahusiano ya kimataifa”

Waziri Mabula amesema kuwa Serikali ya Tanzania inachukua hatua madhubuti ili
kukabiliana na ongezeko kubwa la watu mijini na changamoto za makazi na mabadiliko ya tabianchi, kama sehemu ya Malengo ya Maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals) ambayo kila nchi duniani inatekeleza.
Amesema kuwa takwimu za sensa ya watu na makazi nchini iliyofanyika mwaka 2022 zinaonyesha kuwa asilimia 35 ya Watanzania wanaishi mijini huku kukiwa na ongezeko la uhamiaji mijini la asilimia 4.8 kila mwaka kati ya Watanzania wote 61.7 milioni.
Dk. Mabula pia ameueleza Mkutano huo kuwa Serikali inalenga kuendelea kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na kuhamasisha matumizi ya usafiri usioharibu mazingira, kudhibiti mafuriko, kuweka mipango ya kuifanya miji
iwe salama kwa mazingira na kuweka mipango ya kudhibiti kina cha bahari kisizidi na kuingia nchi kavu.
Sambamba na mipango hiyo amesema serikali itaendelea kuhimiza matumizi bora ya uzalishaji nishati safi na endelevu. Aidha, aliufahamisha mkutano kuwa, serikali imerasimisha makazi kwa asilimia 61 ya makazi yasiyopangwa nchini ambayo kwa sasa yametimia 3,400.
Akasisitiza kuwa mipango yote hiyo aliyoitaja ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya Taifa chini ya makubaliano ya Paris na kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi zinazochochea kwa kiasi kikubwa na idadi kubwa ya watu kuhamia
mijini, gharama zake haziwezi kuondolewa na Serikali peke yake.