MBUNGE MAVUNDE KUANZISHA MASHINDANO YA MICHEZO KWA WANAFUNZI WA SEKONDARI JIJINI DODOMA

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde anatarajia kuanzisha mashindano makubwa ya michezo kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari Jijini Dodoma kwa lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi Jijini Dodoma.

Mavunde ameyasema hayo leo wakati akikabidhi vifaa vya michezo vyenye Thamani ya Tsh 4,000,000 kwa wanafunzi wanamichezo kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambao wanashiriki mashindano ya michezo ya Shule za Sekondari(UMISSETA) katika ngazi ya Mkoa.

“Nawapongeza walimu na wanamichezo wote kwa hatua hii ya kuwaandaa wanafunzi hawa kwa mashindano ya kimkoa.

Leo nipo hapa kuwakabidhi vifaa vya michezo kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya UMISSETA na kuwatakia kila la kheri katika kuiwakilisha vyema Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Kuanzia mwakani 2024,nitaanzisha mashindano makubwa ya michezo mbalimbali kwa kushirikisha shule zote Jijini Dodoma kwa lengo la kuibua na kuendeleza vipaji hapa Jijini Dodoma.

Tunashukuru Mh Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo kwa kuanza ujenzi wa vituo vya michezo hapa Jijini Dodoma ambapo wanafunzi wetu wengi watapata nafasi ya kuweza kuvitumia na kukuza vipaji vyao”Alisema Mavunde

Akitoa maelezo ya awali,Afisa Elimu Sekondari Jiji la Dodoma *Bi. Zainab Abdallah Mohamed * amemshukuru Mbunge Mavunde kwa namna ambavyo amekuwa na mchango mkubwa kukuza michezo katika shule za Sekondari Jijini Dodoma na kuahidi kwamba watafanya vizuri katika mashindano ya UMISSETA ngazi ya mkoa na kuliwakilisha vyema Jiji la Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *