
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ambaye anamuwakilisha Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, atawasilisha katika Mkutano huo wa dunia tamko la Tanzania.
Tamko hili litaonyesha juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania kukabiliana na changamoto za makazi na mabadiliko ya tabianchi, kama sehemu ya malengo ya milenia ambayo kila nchi duniani inatekeleza.
Waziri Mabula atatoa tamko hilo kesho (Juni 6, 2023) kwenye Mkutano Mkuu wa Shirika la Makazi Dunianj unaohudhuriwa na washiriki zaidi ya 5,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani kuwa Mkutano huo unafanyika wakati dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali za makazi zilizosababishwa na COVID 19, mabadiliko ya tabianchi na migogoro ya kivita ambayo imeongeza hali ya umaskini, huduma hafifu za makazi, njaa na mafuriko katika maeneo kadhaa ya dunia.
Waziri Mabula ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri duniani wanaohusika na uendelezaji wa miji na makazi. Mkutano huo unatangulia mkutano Mkuu wa Shirika la Makazi Duniani ulioanza leo Jijini Nairobi ambao kauli mbiu yake ni “hatma ya miji endelevu kupitia ushirikishwaji na uwepo wa mifumo ya mahusiano ya kimataifa”
Wakati huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa(UN- Habitat) Bi. Maimunah Mohd Sharif ameeleza kuwa kufikia mwaka 2030 watu bilioni 3 ambayo ni asilimia 40 ya idadi ya watu duniani watakuwa wakiishi mijini katika makazi yasiyo salama na yasiyokiwa na huduma muhimu.
Hivyo, ili kukabiliana na hali hiyo nchi zote za dunia zinapaswa kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto zitakazotokana na kuongezeka kwa idadi ya watu.
Bi. Maimunah ameyasema hayo alipokuwa akitoa hotuba ya utangulizi ya kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. William Samoei Ruto kufungua Mkutano huo.
Bi Maimunah amesema kuwa changamoto hizo zinahitaji serikali zote za dunia kushiriki kikamilifu kukabiliana nazo ili kufikia malengo ya milenia ya kuwa na miji endelevu, salama na jamii imara.