WAZIRI BASHE AINGILIA KATI MGOGORO WA ARDHI MBEYA ULIODUMU KWA MIAKA 49

Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesitisha zoezi la ujenzi wa mipaka pamoja na nyumba za makazi katika eneo la Sae lenye mgogoro baina ya Wananchi na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ya Jijini Mbeya lililodumu kwa zaidi ya miaka 49 ambalo lina ukubwa wa ekari 67.

Mhe. Bashe ametoa maamuzi hayo leo tarehe 3, Juni 2023 wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Sae Jijini humo ukiwahusisha Wananchi pamoja na Viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homela kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

Akizungumza kwa niaba ya Wananchi hao, Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Dkt. Tulia amesema kuwa ifike wakati sasa kwa Serikali kulimaliza jambo hilo ambalo limedumu kwa muda mrefu ili kila upande ikiwemo Wananchi wake wapate stahiki zao sahihi ikiwa ni pamoja na kuachiwa maeneo yao ama kulipwa fidia ili kupisha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa eneo hilo Ndg. Elius Mwakyusa, amesema wamekuwa wakipata matishio ya mara kwa mara kutoka kwa baadhi ya Askari Polisi wakiwataka wahame kwenye maeneo hayo na ndipo walipoamua kupelea kilio chao kwa Mbunge wao ili awasaidie kuwatafutia ufumbuzi wa kudumu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *