
Mamlakan ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA ) katika kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti 2023 imetabiri uwepo wa hali ya ukavu katika maeneo mengi ya nchi, huku upepo kutoka kusini-mashariki hadi mashariki unatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika Bahari ya Hindi ambao unaweza kusababisha vipindi vya mvua katika maeneo machache ya ukanda wa pwani.
Mikao hiyo ya ukanda wa Pwani ni Mtwara, Lindi, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Akitoa taarifa leo tarehe 26/5/2023 ya mwelekeo wa hali ya hewa kwa kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti, 2023,
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a , amesema kuwa hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo ya nyanda za juu kusini -magharibi pamoja na ukanda wa Ziwa Victoria.
Dkt. Chang’a amesema kuwa Kanda ya Ziwa Victoria, Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu, hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi, huku kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 13 oC na 19 oC.
Amesema kuwa Ukanda wa
Pwani ya Kaskazini, Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi.
“Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 22oC na 26oC kwa maeneo ya mwambao wa pwani na visiwani na kati ya nyuzi joto 19oC na 22oC katika maeneo ya nchi kavu” amesema Dkt. Chang’a.
Hata hivyo ameeleza kuwa maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 19oC.
Amefafanua kuwa kanda ya nyanda za juu kaskazini mashariki, Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi, kiwango hicho kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 13 oC na 21 oC.
“Maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 13 oC. 1.4 Kanda ya magharibi, Mikoa ya Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma, hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15 oC na 19 oC. 1.5” amesema Dkt. Chang’a.
Amesema kuwa kanda ya kati Mikoa ya Singida na Dodoma, hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 14oC na 19oC.
Pia Ukanda wa pwani ya kusini, Mikoa ya Mtwara na Lindi, hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 16 oC na 22 oC.
Kanda ya kusini, Mkoa wa Ruvuma, hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 11oC na 16 oC.
Kanda ya nyanda za juu kusini-magharibi Mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya kusini ya mkoa wa Morogoro, hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 7 oC na 16 oC.
Hata hivyo katika maeneo ya miinuko kiwango hicho kinatarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto 7 oC.
Dkt. Chang’a ametoa tahadhari za kiafya zichukuliwe ili kulinda jamii dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na baridi, vumbi na matumizi ya maji yasiyo safi na salama kutokana na hali ya ukavu inayotarajiwa katika maeneo mengi katika kipindi hicho.
“Maji na malisho yanapaswa kutumika kwa uangalifu ili kupunguza athari zinazotarajiwa, wafugaji kuendelea kuzingatia ratiba za kuogesha mifugo ili kudhibiti magonjwa ya mifugo na kufuata ushauri wa wataalam” amesema Dkt. Chang’a.
Ametoa wito kwa wakulima kuhamasishwa kulima mboga mboga na mazao ya mizizi kama vile viazi katika maeneo oevu na pia katika maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua, huku Sekta za ujenzi, madini na uchukuzi zinaweza kunufaika kutokana na hali ya hewa inayotarajiwa.