KIONGOZI MBIO ZA MWENGE WA UHURU AZINDUA KLABU YA WAPINGA RUSHWA KATIKA SHULE YA SEKONDARI KIBASILA

Na. Noel Rukanuga- DSM

Kiongozi wa Mbio za Mwenge leo tarehe 24/5/2023 amezindua Klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule ya Sekondari Kibasila, huku akiitaka jamii kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya rushwa.

Klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule za Sekondari Kibasila ni miongoni mwa klabu zilizoanzisha na TAKUKURU Mkoa wa Temeke kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanafunzi pamoja na kuhakikisha wanaendelea kutokomeza vitendo vya rushwa nchini.

Akizungumza baada ya kuzindua klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule ya Sekondari Kibasila, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Bw. Abdalla Shaib Kaim, amewapongeza walimu na wanafunzi kwa uwepo wa klabu ya wapinga rushwa shuleni hapo.

Bw. Kaim amesema kuwa rushwa ni adui wa haki, maendeleo pamoja na utoaji wa huduma za kijamii, hivyo kila mmoja anapaswa kutoa ushirikiano katika kuhakikisha malengo tarajiwa yanafikiwa ya kutokomeza vitendo vya rushwa.

“Tuendelee kuwafundisha vijana wetu maadili mema wakiwa Shule pamoja na kutoa taarifa kuhusu uwepo wa vitendo vya rushwa kwa kupiga namba 113 bure” amesema Bw. Kaim.

Akisoma taarifa ya utendaji kwa kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bi. Esther Mkokota, amesema kuwa wanaendelea na utekelezaji wa majukumu yao ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa ufanisi.

Bi. Mkokota amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai 2022 hadi Mei 2023 wamefanikiwa kutoa elimu kwa wananchi 37, 894.

“Tumefanikiwa kutoa elimu kwa njia ya semina, mijadala ya wazi na mikutano pamoja na kutumia vyombo vya habari” amesema Bi. Mkokota.

Amesema kuwa pia wamepokea taarifa 100 kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali kuhusu uwepo wa vitendo vya rushwa na kuzifanyia kazi na kuchukua hatua kupitia dawati la uchunguzi.

Amebainisha kuwa kuna mashauri 18 yanaendelea Mahakamani ya vitendo vya rushwa, mashauri saba yamekamilika, huku Jamhuri ikifanikiwa kushinda kesi sita.

Bi. Mkokota amesema kuwa wamefanikiwa kusimamia miradi 18 ya maendeleo yenye thamani ya Sh 6, 060, 000, 000 na miradi iliyobainika kuwa na kasoro ushauri ulitolewa na namna bora ya kufanya maboresho.

“Tunaendelea kushirikiana na wananchi pamoja na wadau mbalimbali kupitia PROGRAMU YA TAKUKURU RAFIKI iliyoanzishwa ili kukabiliana na tatizo la utoaji wa rushwa katika huduma za kijamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo” amesema Bi. Mkokota.

Mlezi wa Klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule ya Sekondari Kibasila, Mwalimu Imelda Mwinyi, amesema kuwa klabu hiyo ilianzishwa mwaka 2017 kwa ajili kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu vitendo vya rushwa pamoja na kuwafundisha kufanya kazi kwa bidii, wawe maadili, nidhamu pamoja na hofu ya Mungu.

Mwalimu Mwinyi amesema kuwa elimu hiyo inamsaidia mwanafunzi kuepukana na vishawishi vya kutoa rushwa pamoja na kutoa fursa kwenda kuelimisha jamii pamoja na kufanya programu mbalimbali na kuleta ripoti.

“Hatuchukua mwanachama kama mwanachama lazima tuangie maadili yao ili waweze kuwa mfano mzuri wa kuigwa na wengine, awe kioo kwa wezake” amesema Mwalimu Mwinyi.

Mwanachama wa Klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule ya Sekondari Kibasila, Mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza Lukman Salim, amesema kuwa klabu ya wapinga rushwa imekuwa msaada kwao kwani wamekuwa wakipata elimu ya namna bora ya Kuzuia na Kupambana na rushwa.

“Rushwa ni adui wa haki, imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya nchi, nawashauri wanafunzi wajiunge na klabu ya wapinga rushwa kwani ni muhimu katika maisha yetu” amesema Salim.

Kauli mbiu ya mwaka huu Mbio za Mwenge wa Uhuru : Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *