RASIMU YA MKAKATI WA KUENDELEZA TASNIA YA MBOLEA NCHINI YAJADILIWA,WADAU WATOA MAONI YAO

Mkurugenzi Myendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo (kulia) akiwa katika meza na watumishi wa Mamlaka, wakifuatilia maelezo wakati wa kikao cha wadau kujadili na kutoa maoni juu ya wasilisho la Rasimu ya Mkakati wa Kuendeleza Tasnia ya Mbolea nchini. Wa kwanza kushoto ni Mratibu wa Mradi wa Sera Bora, Prof. David Nyange
Mdau wa Tasnia ya mbolea Timoth Mbaga akichangia mada
Watendaji wa serikali na wadau wa tasnia ya mbolea nchini wakifuatilia wasilisho la rasimu ya kwanza ya Mkakati wa Kuendeleza Tasnia ya Mbolea uliofanyika tarehe 19 Mei, 2023 katika ukumbi wa hoteli ya Protea Jijini Dar Es Salaam.
Wadau wa tasnia ya mbolea wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kujadili na kutoa maoni yao ya kuboresha rasimu ya awali ya Mkakati wa Kuendeleza Tasnia ya Mbolea nchini uliofanyika tarehe 19 Mei, 2023 katika Hoteli ya Protea Jijini Dar Es Salaam.

Wadau wa mbolea nchini wamekutana na kujadili rasimu ya kwanza ya Mkakati wa Kuendeleza Tasnia ya Mbolea nchini wenye lengo la kupunguza changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia hiyo ili kuifanya ikuze Sekta ya kilimo nchini.

Changamoto zinazoikabili tasnia ya mbolea ni kama mabadiliko ya mara kwa mara ya bei ya mbolea, mbolea kutopatikana kwa wakati kwa mkulima, matumizi madogo ya mbolea na visaidizi vyake, uwekezaji mdogo katika uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi, ukosefu wa mitaji, ufinyu wa mtandao wa mawakala wa mbolea vijijini, ubovu wa barabara, upungufu wa vifungashio na maghala, uhaba wa tafiti za mbolea , uelewa mdogo wa teknolojia za kupima udongo, na matumizi madogo ya malighafi za kutengenezea mbolea zinazopatikana ndani ya nchi.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 19 Mei, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya udhibiti wa Mbolea nchini, Dkt. Stephan Ngailo wakati akifungua kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Willingtong katika hoteli ya Protea Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Ngailo amesema ongezeko la viwanda vya mbolea nchini litaihakikishia nchi upatikanaji wa mbolea zenye bei himilivu na hivyo kupelekea ongezeko la matumizi ya mbolea kwa wakulima na baadaye kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Tunatarajia uzalishaji na upatikanaji wa mbolea ukiongezeka bei ya mbolea itakuwa himilivu na kuchangia kuongeza matumizi ya mbolea na uzalishaji wa mkulima mmoja mmoja kuongezeka na baadaye kushusha bei ya nafaka sokoni.

Dkt. Ngailo ameongeza kuwa, Tasnia ya mbolea ni eneo muhimu liloainishwa na Serikali katika kuongeza tija na uzalishaji katika kilimo na kubainisha kuwa kufuatia umuhimu huo Mamlaka imeona vema kuja na Mkakati wa kuendeleza tasnia ya mbolea ili kuweka mipango mathubuti ya namna bora kusimamia tasnia hiyo kwa matokeo chanya.

‘‘Rasimu ya Mkakati iliyoandaliwa imejumuisha masuala ya kitaifa na kimataifa na jitahada zinazohusiana na kuendeleza tasnia ya mbolea, kilimo na mipango ya maendeleo ya kiuchumi ya muda mfupi, wa kati na mrefu ili kuhakikisha TFRA kama mdhibiti na wadau wengine wanajiandaa na mabadiliko muhimu katika tasnia ya mbolea’’ Dkt. Ngailo aliongeza.

Akiwasilisha rasimu hiyo, Mratibu wa Mradi wa Sera Bora, Prof. David Nyange, amewaomba wadau kuchangia maoni yao ili kuwezesha kufikia matarajio ya ukuaji wa tasnia ya mbolea.

Ameeleza kuwa, ili nchi kujitosheleza na kufanikiwa kufanyabiashara ya mbolea nje ya nchi, ziada ya uzalishaji wa mbolea kwenye viwanda vya ndani unapaswa kuwa ni asilimia 50 ya mahitaji ya mbolea kwa mwaka.

Kwa upande wake Meneja Mauzo wa Kampuni la Mbolea Minjingu, Dkt. Mshindo Msola ameeleza kuwa, ili kukuza tasnia ya mbolea nchi inapaswa kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi na badala yake iendelee kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya ndani.

Ameongeza kuwa, ili kuwa na kilimo chenye tija matumizi ya mbolea ni lazima na kusisitiza matumizi hayo ni lazima yazingatie afya ya udongo pamoja na mahitaji ya zao husika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *