TARURA MKOA WA SIMIYU KAZI INAENDELEA

UWEKEZAJI mkubwa wa fedha za miundombinu ya barabara za wilaya zinazohudumiwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Simiyu umewezesha barabara nzuri kuongezeka kwa asilimia 40.64.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Simiyu Mhandisi Gaston Paschal anasema mafanikio hayo yamepatikana katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

TARURA Mkoa wa Simiyu inahudumia mtandao wa Barabara wenye jumla ya kilomita 4,163.83 na kati ya hizo kilomita 1,690.64 za barabara ambazo sawa na asilimia 40.64 ziko katika hali nzuri.

Pia kilomita 1,346.83 za barabara sawa na asilimia 32.34 ni za wastani wakati kilomita 1,126.38 za barabara sawa na asilimia 27.05 si za kuridhisha.

Aidha, kilomita 24.22 ni barabara za lami ambazo ni sawa na asilimia 0.58, kilomita 1,776.66 ni za changarawe sawa na asilimia 42.67 huku mtandao wa barabara za udongo ni kilomita 2,362.95 sawa na asilimia 56.75 wakati madaraja ni 101 na makalavati yako 912.

Akizungumzia mafanikio kwa kipindi cha miaka miwili ya mwaka 2021/22 hadi 2022/23, Meneja wa TARURA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Gaston Paschal anasema zaidi ya asilimia 70 ya mtandao wa barabara hizo zinapitika.

Anasema barabara nzuri zimeongezeka kutoka kilomita 931 hadi kilomita 1690.64 sawa na asilimia 40.64 wakati barabara zenye hali ya kuridhisha zimepungua kutoka kilomita 1,720 hadi kufikia kilomita 1,346.83 sawa na asilimia 32.34.

Mhandisi Paschal anasema pia barabara zenye hali isiyoridhisha zimepungua kutoka kilomita 1,512.71 hadi kufikia kilomita 1,126.38 sawa na asilimia 27.05 huku madaraja yameongezeka kutoka 72 hadi kufikia madaraja 101 wakati idadi ya makalavati imeongezeka kutoka 423 hadi kufikia makalavati 912.

Anasema pia TARURA Simiyu imepata magari ya usimamizi 3 katika Wilaya za Maswa, Itilima na Busega, taa 131 za barabarani zimefungwa katika wilaya za Itilima, Maswa, Bariadi na Meatu huku mifereji kilomita ya Maji ya mvua jumla ya kilomita 7.5 zimejengwa.

“Pia mtandao wa barabara mpya wenye jumla ya kilomita 112.30 zimefunguliwa katika uwekezaji huo,” anasema Mhandisi Paschal.

Akizungumzia ongezeko la bajeti ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara, Mhandisi Paschal anasema ndani ya miaka miwili ya Mheshimiwa Rais Samia kuwa madarakani bajeti imeongezeka kutoka Sh bilioni 5.88 mwaka 2020/2021 hadi kufikia Sh billioni 18.22 mwaka 2021/2022 sawa na asilimia 218 na kwa mwaka 2022/23 zimetengwa zaidi ya Sh bilioni 18.

“Ongezeko hili la bajeti ya matengenezo ya barabara zinajumuisha fedha kutoka vyanzo vitatu vya mapato ambavyo ni fedha za matengenezo, fedha za jimbo pamoja na zile zitokanazo na tozo ya mafuta.”

Aidha, Mhandisi Paschal anasema Wakala umepanga kuzifanyia matengenezo barabara zote zenye hali nzuri na wastani ili ziweze kudumu kwa muda unaostahili.

“Pia tutahakikisha sehemu zote za barabara zenye vikwazo vya kupitika zitafanyiwa matengenezo ili ziweze kupitika.”

“Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini Mkoa wa Simiyu tunatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassani kwa kutuongezea kiasi kikubwa cha bajeti ya matengenezo ya babarabara kiasi ambacho kitazidi kuimarisha barabara zetu za vijijini na mijini.”
(mwisho)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *