NDEJEMBI ASISITIZA TARURA KUTUMIA TEKNOLOJIA MBADALA

OR- TAMISEMI

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb) ameisisitiza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuweka kipaumbele katika matumizi ya teknolojia mbadala katika ujenzi wa barabara na madaraja.

Ameyasema hayo leo tarehe 02 Mei 2023 jijini Dodoma wakati alipofanya ziara yake ya kwanza katika Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na kuzungumza na Menejimenti pamoja na watumishi.

“Mmekuwa mkimsikia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akisisitiza sana matumizi ya teknolojia mbadala , kwahiyo hakikisheni mnaweka jitihada katika utekelezaji wa maelekezo hayo ili kupunguza gharama za ujenzi” amesema Ndejembi.

Amesema matumizi ya teknolojia mbadala yanaleta unafuu wa gharama za ujenzi na matengenezo ya barabara na pia husaidia kuhifadhi mazingira.

Aidha, Ndejembi amemtaka Mtendaji Mkuu wa TARURA kuhakikisha kazi zote za kujenga miundombinu ya barabara na miundombinu mingine zitolewe kwa wakandarasi wenye uwezo wa kutekeleza miradi kwa ubora na kukamilisha kwa wakati.

Aidha, Ndejembi amewataka Watumishi wa TARURA kufanya kazi kwa uadilifu wakati wakutekeleza majukumu yao na kusimamia vyema rasilimali fedha inayotolewa na Serikali.

Kadhalika, ameipongeza TARURA kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara ambayo inatafsiri kwa vitendo maono ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor H. Seff amesema katika matumizi ya malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi, kufikia mwezi Machi 2023 TARURA imejenga madaraja 163 ya mawe yenye thamani ya Shilingi bilioni 8.7 ambapo gharama imepungua kwa zaidi ya asilimia 50.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *