WAZIRI MKUU MAJALIWA ATOA MAELEKEZO KWA MAMLAKA ZA SERIKALI NA MAAGIZO TAMISEMI, MALIASILI NA UTALII

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametoa ufafanuzi kuhusu mwenendo wa matukio yanayoendelea hapa nchini ikiwemo maswala ya uhifadhi athari zinazotokana na kuongezeka kwa idadi ya wanyama waharibifu na wakali, hali inayosababisha kudorora kwa mahusiano kati ya wananchi na mamlaka zinazohusika kusimamia uhifadhi huo.


Mheshimiwa Majaliwa ametoa ufafanuzi huo katika kipindi cha Maswali ya papo kwa papo Bungeni leo Aprili 27, 2023 jijini Dodoma ambapo amesema Ongezeko la shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo, Ufugaji na Makazi sambamba na kuimarika kwa shughuli za uhifadhi kumechangia kwa kiasi kikubwa changamoto hizo.


“Shughuli za kibinadamu zimechangia wananchi kuingia katika maeneo ya hifadhi kwa kujua ama kwa kutokujua, kwa kuendeleza shughuli za kilimo na ufugaji na makazi, kwa upande mwingine kuimarika kwa shughuli za uhifadhi kumewezesha baadhi ya wanyama kama vile Tembo kuongezeka na hivyo kusababisha uharibifu wa mazao, ulemavu, na hata vifo kwa baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo yanayopakana na hifadhi” Mhe. Majaliwa

Amebainisha kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazoibuliwa ni pamoja na migogoro ya ardhi kati ya wananchi na hifadhi na kutokuwepo kwa mahusiano mazuri kati yao na Mamlaka za Uhifadhi kwa kutambua hilo Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuendelea kuthibiti uvamizi katika maeneo ya uhifadhi, kutatua migogoro inayohusiana na mwingiliano wa shughuli za wananchi na uhifadhi, pamoja na kuimarisha uhusiano bora kati ya uhifadhi na maendeleo.

“Ninatambua uwepo wa mgogoro katika Wilaya ya Tarime na Serengeti. Pamoja na hatua kadhaa zilizoanza kuchukuliwa na Serikali, nitumie nafasi hii kuwaagiza Mawaziri wa TAMISEMI na Maliasili na Utalii kuhakikisha wanakwenda kukutana na wananchi katika vijiji  husika kwa ajili ya kutoa elimu na ufafanuzi” Mhe. Majaliwa

Aidha ametoa maelekezo kwa mamlaka mbalimbali, kusimamia Oparesheni zote zifanyike baada ya wananchi wa eneo husika kushirikishwa na kupewa taarifa zakutosha.

“Wahifadhi wahakikishe wanazuia mapema wananchi kuanzisha shughuli za kilimo, ufugaji na makazi ndani ya hifadhi ili kuepuka uhitaji wa kuondoa shughuli ambazo zimeshaanzishwa, Wananchi wenye malalamiko ya kunyang’anywa mali/mifugo, kujeruhiwa wahakikishe wanatoa taarifa ya matukio hayo kwa wakati katika vituo vya polisi na Mamlaka za Wilaya ili iwe rahisi kwa Serikali kuchukua hatua, Wahifadhi waimarishe mahusiano ya ujirani mwema na kutoa elimu kwa wananchi wanaopakana na hifadhi kuhusu manufaa ya uhifadhi endelevu” Mhe. Majaliwa

“Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya zishirikishwe kikamilifu pale penye tuhuma dhidi ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi, Sheria ya Uhifadhi Sura 282 ifanyiwe mapitio ili kuweka ulinganifu wa kiasi kinachopaswa kutozwa kama adhabu na kubainisha wazi kama kiasi tajwa kitahusu mfugo mmoja au kundi zima. “Mhe. Majaliwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *