UJENZI WA BARABARA YA UVINZA – MALAGARASI (KM 51.1) WAFIKIA ASILIMIA 31

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Ngoko Mirumbe, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara ya Uvinza hadi Malagarasi yenye urefu wa Kilometa 51.1 kwa kiwango cha lami Mkoani Kigoma.

Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imesema ujenzi wa barabara ya Malagarasi-Ilunde-Uvinza yenye urefu wa kilometa 51.1 kwa kiwango cha lami umefikia asilimia 31 ya utekelezaji wake na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2023. 
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Ngoko Mirumbe wakati wa Ziara ya Waandishi wa Habari katika miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa mkoani humo. 
Mhandisi Mirumbe amesema Serikali imelenga kuhakikisha inaiunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za lami jitihada ambazo zinajidhihirisha kwa uwepo wa miradi mingi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ndani ya mkoa wa Kigoma na hivyo kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji ili kuchangia uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla. 

Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara Uvinza hadi Malagarasi yenye urefu wa Kilometa 51.1 inayojengwa kwa kiwango cha lami, Mkoani Kigoma.


“Ujenzi wa barabara hii ni moja ya uwepo wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa kwa kasi ndani ya mkoa ambayo inaashiria kwamba ndani ya muda mchache sana kutoka sasa Mkoa wa Kigoma utakuwa umeshaunganishwa kwa miundombinu ya barabara za kiwango cha lami”amefafanua Mhandisi Mirumbe

 
Amesema kuwa mradi wa Malagarasi-Ilunde-Uvinza ni sehemu ya barabara kutoka Kigoma-Uvinza-Malagarasi yenye urefu wa kilometa 212 ambapo kati ya hiyo kilometa 105 kutoka Kigoma hadi Uvinza zikiwa zimeshajengwa kwa kiwango lami tayari na sasa hadi kuelekea Tabora zimesalia Kilometa 61 ambazo zote mkandarasi yuko site akiendelea na kazi. 


Amesema ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 62 na mradi unatekelezwa kupitia mkandarasi STECOL Cooperation chini ya Mhandisi Mshauri Norplan Tanzania 
Aidha amebainisha kuwa mradi umeajiri wafanyakazi 216 kati yao wafanyakazi wageni wakiwa ni 21 pekee. 
Naye Kaimu Mhandisi Mkazi, Mhandisi Yusuf Karera amesema, hadi sasa kazi mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo zimefanyika ikiwemo kujenga makaravati 22 huku makaravati madogo yakiwa ni 19 na makaravati makubwa matatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *