NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.

Serikali imetakiwa kufanya uwekezaji wa kununua vifaa vya kisasa pamoja na kutumia wataalamu jambo ambalo litasaidia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutekeleza majukumu kwa ufanisi, kwani taasisi hiyo ni mtambuka inayotegemewa na sekta mbalimbali nchini kwa ajili ya kufanikisha shughuli mbalimbali za uchumi.
Akifanya mahojiano maalum na mwandishi wetu jijini Dar es Salaam, Mtaalamu wa Uchumi Profesa Humphery Moshi, amesema kuwa TMA ni sekta mtambuka inayotegemewa na taasisi za serikali na binafsi katika kufanikisha shughuli za maendelao.
“Naipongeza TMA kwa kutoa utabiri wa taarifa za hali ya hewa kwa usahihi hadi kufika asilimia 88.5, ni taarifa rafiki kwa wadua wa uchumi kwani taarifa za hali ya hewa zimekuwa zikitumika katika kupanga na kutekeleza shughuli za uchumi” Profesa Moshi.
Amesema kuwa bado kunaitajika usahihi wa taarifa za hali ya hewa hadi kufikia asilimia 99 jambo ambalo litasaidia kujua ukweli wa hali ya hewa kila eneo kulingana na mazingira ya utabiri unavyosema.
“Ukienda nchi mbalimbali duniani ikiwemo Marekani ambazo zimepiga hatua kimaendeleo utabiri wao unaeleza taarifa zote ikiwemo mvua itanyesha sehemu fulani, muda fulani na kiasi fulani cha mvua” amesema Profesa Moshi.
Ameeleza kuwa wakati umefika TMA kuweka mikakati kwa kushirikiana na nchi ambazo zimepiga hatua kwa kubadilishana uzoefu wa wataalamu na teknolojia ya kisasa ili utabiri taarifa za hali ya hewa uwe na tija zaidi kuliko ulivyokuwa sasa.
Hata hivyo ameeleza kuwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa serikali na wadau mbalimbali wanapaswa kufanya maandalizi ili kukabiliana changamoto zinazoweza kujitokeza.
“Kulikuwa na ukame kwa kipindi cha mwezi mmoja tumeona nchi ilivyoangaika, ipo haja ya kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji na ukiangalia Mungu ametujalia kutokana tuna maziwa makubwa matatu ambayo tunaweza kuyatumia” amesema Profesa Moshi.
Amesema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yana madhara makubwa katika sekta ya uchumi, kwani yanasababisha kupunga kwa uzalishaji wa mazao hasa katika kipindi cha ukame.
Amesema kuwa serikali inakosa kodi kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa mazao, kwani kiasi ambacho kilipaswa kulipwa awali cha kodi kitapungu kutokana mabadiliko ya hali ya hewa.
“Mtu alikuwa analipa kodi Sh. 10,000, lakini kutokana na uzalishaji wa mazao umepungua anajikuta analipa 2,000, hivyo bajeti ya serikali lazima iathirike kutokana asilimia kubwa wanategemea kodi” amesema Profesa Moshi.
Profesa Moshi ambaye aliwai kuwa mshauri wa serikali ya Zanzibar katika sekta ya uchumi, amesema kuwa yapo majenga mengi yanajitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa hali ambayo serikali inajikuta inapunguza bajeti yake katika ujenzi wa miundombinu ya barabara au sekta ya afya ili waweze kutatua tatizo ambalo lipo mbele yao.
“Wakati umefika kwa serikali kutenga bajeti kwa ajili ya kushughulikia athari zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa” amesema Profesa Moshi.
Amefafanua kuwa mabadiliko ya hali ya hewa duniani yamechangiwa nchi tatu ambazo uchumi wao unategemea viwanda ikiwemo Marekani, India na China, lakini nchi za afrika ndiyo zinaathirika zaidi kutokana zinategemea kilimo.
Amesema kuwa asilimia 64 za kaya nchi za Afrika zinategemea kilimo ili kuendesha maisha yao ya kila siku, hivyo wakishindwa kuvuna mazao ya kutosha kipato chao kitapungua.
“Mazao yakizalisha kidogo bei inakuwa kubwa sokoni na kusababisha mfumuko wa bei kuwa mkubwa na kupelekea thamani ya fedha kushuka kwa kiasi kikubwa” amesema Profesa Moshi.
Ameeleza kuwa kutokana na kukosekana kwa chakula watu wanaweza kula mlo mmoja kwa siku na kupelekea afya zao kuwa duni.
“Hatua stahiki zinapaswa kuchukulia ikiwemo kutunza vyanzo vya maji kwa kupanda miti pamoja na kuhakikisha sheria kali zinachukuliwa kwa watu watakaobainika waharibifu wa vyanzo vya maji” amesema Profesa.
Hata hivyo katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kwa ujumla vimeongezeka na kufikia asilimia 88.5
Imeelezwa kuwa kiwango cha usahihi wa utabiri kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) cha asilimia 70 jamba ambalo linaelezwa kuwa mafanikio hayo yametokana na jitiada zilizofanywa na TMA.
Akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema kuwa wadau mbalimbali nchini wanatakiwa kuchukua tahadhari kuhusu taarifa za hali ya hewa ambazo zinaonesha zinaweza kuleta madhara.
Amesema kuwa serikali kwa ushirikiana na wadau mbalimbali wanapaswa kuchukua hatua ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
“Mamlaka ya miji inapaswa kuifadhi maji yanayopatikana kutokana na mvua pamoja na kuweka miundombinu rafiki ya kuifadhi maji na kuweza kuyatumia katika wakati ambao unafaa” amesema Dkt. Chang’a