Jeshi la Kujenga Taifa JKT limesema limejipanga kuhakikisha linapunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa upatikanaji wa mafuta ya kupikia unaotokea mara kwa mara hapa nchini kwa kuhakikisha wanazalisha kwa wingi mazao ya mafuta kama alizeti na michikichi na kuhakikisha wanaongeza upatikanaji wa mbegu bora za mazao hayo hapa nchini.
Hayo yamebainishwa Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma na Mkuu wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena wakati alipotembelea shamba la uzalishaji wa mbegu bora za alizeti shamba lenye ukubwa wa ekari 500 lililopo Chenene Chamwino.
Amesema Taifa limekuwa na uhitaji wa tani laki sita na hamsini elfu (650,000) za mafuta ya kupikia na upatikanaji ni tani laki mbili na tisini elfu (290,000) na kuna upungufu wa tani laki tatu na sitini elfu(360,000) hivyo wamejipanga kuhakiki wanaondoa upungufu huo.

“Kama JKT tumejikita katika kilimo, Mifugo na Uvuvi na kwa upande wa chakula tumejitosheleza sasa tunataka tujikite katika uzalishaji wa mazao ya mafuta na hapa tumeanza na uzalishaji wa mbegu za zao la alizeti ili kuhakikisha mbegu bora inapatikana JKT na wakulima wapate mbegu bora” amesema.
Amesema kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa kilimo TARI kituo cha Ilonga walifanya utafiti wa udongo na kuthibitika kuwa na kiwango kinachotakiwa katika uzalishaji wa zao la alizeti na kuhakikisha mbegu inayozalishwa ni ya uhakika itakayomsaidia mkulima tofauti na mbegu nyingine zinazotumika msimu mmoja.
“Pia kwa kushirikiana na wataalamu wa Kilimo katika kudhibiti magugu na wadudu waharibifu ili kuhakikisha tunapata mbegu bora, pia tunashirikiana na wataalamu wa hali ya hewa ili kuwa na mazao ya uhakika bila kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi” amesema.

Ameongeza kuwa “ ili kuwa na kilimo cha uhakika katika eneo hili tutatengeneza mabwawa ili kuhifadhi maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji wakati tunajiandaa kutengeneza miondombinu ya umwagiliaji katika eneo hilo tuwe na kilimo cha uhakika” amesema.
Amebainisha kuwa kwa upande wa zao la mchikichi katika kikosi 821 KJ Kigoma zimelimwa ekari 800 za mbegu za msingi wakati ekari 1200 zikiandaliwa lengo ni kufikia uzalishaji katika ekari 2000 zitakazozalisha mbegu za Mchikichi zitakazo tumika katika Halmashauri zinazolima zao la mchikichi.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kutoka JKT Kanali Peter Lushika amesema katika ekari 500 zilizolimwa zitazalishwa tani 600 za mbegu za alizeti huku lengo ni kufikia tani 1300 hadi tani 1500 za mbegu bora za alizeti.
Amesema mara baada ya kuzalisha mbegu za alizeti za kutosha JKT watafungua mashamba ya zao la alizeti ili kuongeza uzalishaji wa zao hili lengo ni kufikia ekari 5000 za mashamba ya alizeti.
Nae Kaimu Kamanda wa kikosi cha 834KJ Makutopora Meja James Macheta amesema katika eneo hilo kuna shamba la ukubwa wa ekari 1000 na lilianza kuandaliwa mwezi wa 10 na kupandwa mwezi Disemba, 2022 na ekari 200 zimelimwa katika eneo la Wilaya ya Kongwa.

Katika hatua nyingine amesema uzalishaji katika mashamba hayo vijana wa kujitolea wameshirikishwa kwa asilimia 100 katika ngazi zote ikiwa ni kuwajengea uwezo na kuwapa ujuzi.
Nao baadhi ya vijana walioshiriki katika kilimo Abdul Mmasi amesema kupitia kilimo hicho wamejifunza hatua mbalimbali ambazo zitawasaidia mara baada ya kuhitimu mafunzo hali itakayowasaidia kuendesha uchumi wao.
“Mafunzo hayo ni mazuri yatatusaidia mimi nina digree(Shahada) lakini nikiwa katika mafunzo haya nimejifunza hatua kwa hatua shughuli za kilimo mafunzo yatanisaidia nikimaliza mafunzo nitajikita katika kilimo” amesema Mmasi.