Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad H. Chande ameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kazi inayofanyika, ikiwa ni pamoja na jitihada zilizopelekea kuwasilisha mswada wa mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, na kuokoa fedha kwa kuingilia kati michakato ya ununuzi wa umma ambayo inaonesha viashiria vya kutopatikana kwa thamani ya fedha.

Ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua Mkutano wa Tatu wa Baraza la Nne la Wafanyakazi wa PPRA, jijini Dodoma.
Alisema kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ana imani kubwa kwa PPRA, hivyo akaitaka kuhakikisha haimuangushi mkuu wa nchi.
Pia, Naibu Waziri ameipongeza PPRA kwa kusimamia ujenzi wa mfumo mpya wa ununuzi wa umma kwa njia ya kielektroni, kazi inayofanywa na wataalam wa ndani ya nchi.
Naibu Waziri wa Fedha pia ameiagiza PPRA kuhakikisha kuwa baada ya kufanyika mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na kuanzishwa mfumo mpya, watoe elimu kwa uwanda mkubwa kwa wadau wa ununuzi nchini.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Bw. Eliakim Maswi alikuwa na ujumbe kwa Naibu Waziri, ikiwa ni pamoja na shukurani kwa Serikali.
