
Mbunge wa Viti Maalum Dodoma, Mhe. Fatma Toufiq amesisitiza kuwa wanawake wanahitaji kujikwamua kiuchumi ili kufanikisha watoto kupata malazi na mavazi pamoja na kuhakikisha familia haitetereki.
Ameyasema hayo leo April 08, 2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza na Kikundi cha Wanawake cha Ari Mpya, Kasi mpya na Nguvu mpya kutoka Kata ya Kisese Wilayani Kondoa, Mkoani Dodoma ambacho kimekuwa kikichukua mikopo ya asilimia 10 katika Halmashauri na kuirejesha kwa wakati.

Pamoja na hayo, Mbunge Toufiq ametoa msaada wa Vifaa vya kushonea nguo ili kikundi hicho kiweze kushona na kuuza ili kujinufaisha huku akiahidi kuongeza msaada zaidi
“Mama akijikwamua kiuchumi familia haiwezi kutetereka, kwahiyo unakuta Baba analeta kidogo cha kwake na Mama nae analeta cha kwake, basi maisha yanaendelea.na sisi ni miongoni mwa sera ya Chama cha Mapinduzi kuhakikisha wanawake wengi tunajikwamua kiuchumi na ndio maana Bunge, Serikali vikaamua kupitisha Sheria ili kusudi wanawake kuweza kupata mikopo na kujikwamua kiuchumi.”Amesema Mbunge Toufiq.

Mbunge huyo ameeleza kuwa amewiwa na Kikundi hicho cha wanawake baada ya kupata Taarifa kuwa kimekuwa kikikopa na kurejesha, hivyo kama ilivyo ada yake kama Mbunge wa Dodoma kuhakikisha anaisaidia jamii akaona hana budi kuweza kutoa msaada kwa kikundi hicho ili kiweze kujiendesha zaidi.

Kikundi hicho kinamiliki Cherehani za kushonea na kimekuwa kikishona na kuuza mavazi ya aina mbalimbali.
