WAKAZI WA TANGA WAPONGEZWA KUKIPAMBANIA CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA KUPATA KIWANJA CHA KUJENGA KAMPASI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewapongeza wakazi wa Majani ya Chai Kata ya Maweni jijini Tanga kwa kukipambania Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) kupata eneo la kujenga kampasi itakayokuwa na manufaa ya vizazi vyao, kwa
wakazi wa mkoa huo na Watanzania wote watakaopata fursa ya kupata elimu katika kampasi hiyo pindi ujenzi wake utakapokamilika.
Mhe. Jenista ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na wananchi wa Majani ya Chai Kata ya Maweni jijini Tanga alipoenda kuwatembelea kwa lengo la kuwashukuru kwa kukiunga mkono Chuo cha Utumishi wa Umma kupata umiliki wa kiwanja ili kujenga kampasi jijini humo.

Mhe. Jenista amesema kuwa, wakazi wa Majani ya Chai jijini Tanga wametoa somo kwa Watanzania kwani maeneo mengine, Serikali ikitaka kujenga miundombinu endelevu kwenye eneo lenye mgogoro wa ardhi mara nyingi wananchi wanakuwa upande wa wanaodai kumiliki viwanja licha ya kushindwa kuviendeleza, hivyo wananchi wa Majani ya Chai wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kupambania ujenzi wa chuo kwa manufaa ya taifa.
“Nimefurahishwa sana na uamuzi wenu wa kulilinda na kulipambania eneo hili na hatimaye Chuo cha Utumishi wa Umma kimepata kiwanja cha kujenga kampasi na kuongeza kuwa, limekuwa ni somo tosha ya namna ya kuisaidia Serikali kupata eneo la kujenga miundombinu yenye tija kwa Serikali na wananchi pia,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista amesema, changamoto iliyokuwepo ilikuwa ni upatikanaji wa eneo la kujenga kampasi ya chuo jijini Tanga, hivyo amemshukuru Kamishna wa Ardhi jijini Tanga kwa kutoa taarifa rasmi kuwa kiwanja hicho ni mali ya Chuo cha Utumishi wa Umma mara baada ya kufanyika kwa mchakato wote wa kisheria wa umilikishaji ardhi kwenye eneo lililokuwa na mgogoro.

“Tumejipanga kujenga kampasi yetu wenyewe kwani tunapanga jengo la kuendesha shughuli za chuo ambalo linatugharimu shilingi milioni 84 kwa mwaka, hivyo leo wananchi wa Majani ya Chai mmeokoa fedha hiyo ya Serikali na kuiwezesha Serikali kutekeleza mpango wa kujenga uwezo wa rasilimali watu
iliyonayo kupitia mafunzo yatakayotolewa na kampasi hiyo kwa watumishi wa umma,” Mhe. Jenista amefafanua.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Hashim Mgandilwa amesema wananchi wa eneo hilo wametekeleza wajibu wao kwa kukipambania Chuo cha Utumishi wa umma kupata eneo la kujenga kampasi jijini Tanga, hivyo amewataka kuendelea kulilinda eneo hilo mpaka ujenzi utakapokamilika.

Naye, Diwani wa Kata ya Maweni, Mhe. Joseph Kolivasi amemshukuru Mhe. Jenista kwa kuwatembelea wananchi wa kata yake na kuongeza kuwa, anaamimi kuwa Kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanga itaanza kujengwa mapema iwezekenavyo na si kujengwa katika eneo lingine kama ambavyo wananchi wa eneo analolitawala wanavyotarajia.
Mmoja wa wakazi wa Kata ya Maweni, Mzee Abdallah Kilo amesema amefurahia kitendo cha Chuo cha Utumishi wa Umma kupewa umiliki wa eneo hilo ili kujenga kampasi kwa manufaa ya kizazi kijacho, kwani ndio jambo ambalo yeye na wenzie wamekuwa wakilipambania kwa nguvu zao zote.

Kaimu Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Dkt. Ernest Mabonesho amewashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kuunga mkono jitihada za chuo chake kupata kiwanja kwa ajili ya kujenga kampasi jijini Tanga na kuongeza kuwa eneo hilo limepatikana kwa jitihada za
wananchi hao.
Dkt. Mabonesho amemshukuru Kamishna wa Ardhi kwa kukamilisha taratibu za kisheria zilizokiwezesha chuo chake kumiliki kiwanja hicho kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi ya Tanga.
Sanjari na hilo, amemshukuru Mhe. Jenista Mhagama kwa uamuzi wake wa kuwatembelea wananchi wa eneo hilo ili kuwashukuru kwa mchango wao katika upatikanaji wa kiwanja hicho.
Chuo cha Utumishi wa Umma kimemilikishwa eneo la ekari 12 kwa ajili ya ujenzi wa kampasi yake jijini Tanga, kampasi inayotarajiwa kutoa mchango wa kujenga uwezo wa kiutendaji wa rasilimaliwatu ya taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *