WAFUGAJI WATAKIWA KUACHA KUWAPELEKA WATOTO SEHEMU ZA MACHUNGO

Wafugaji kote nchini wametakiwa kuacha kuwatumia watoto wadogo kwa ajili ya kwenda kuchunga
mifugo hali inayopelekea kuongezeka kwa matukio ya wizi wa mifugo.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia wizi wa mifugo Nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Simon Pasua
ameyasema hayo leo wakati alipotembelea Kijiji Rozilini kilichopo katika kata ya Enduimet wilaya ya
Siha Mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kutoa elimu ya kuhamasisha wananchi kuhusiana namna ya kuzuia
wizi wa mifugo.
Kamanda Pasua amebainisha kuwa pindi watoto wanapotumika kuchunga mifugo inapelekea
kuongezeka kwa matukio ya wizi wa mifugo hiyo kwa sababu hawana uwezo wa kukabiliana na wahalifu
pindi wanapojitokeza.

Sambamba na hilo ACP Pasua amefafanua kuwa kwa kipindi cha kuanzia mwezi januari hadi machi
mwaka huu jumla ya watuhumiwa 372 walikamatwa wakiwa na mifugo 3,192 ya wizi.

Aliendelea kufafanua kuwa watuhumiwa 116 kati ya waliokamatwa walifikishwa mahakamani ambapo
walipatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela vifungo mbalimhali.
Aidha ametoa onyo kwa watu wachache wanaojihusisha na uhalifu hususani wizi wa mifugo kuacha
mara moja kwani wataendelea kuwakamata na kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.
Naye Bwana John Ndikilo ambaye ni mkazi wa kijiji hicho amewatoa woto kwa wafugaji wenzake kuacha
kuwapeleka watoto sehemu za kuchungia mifugo kwani mbali na kuhatarisha usalama pamoja na
mifugo hiyo pia wanakosa haki ya msingi ya kupata elimu.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Rosilini-A bwana Luka Ngemoryo amesema kijiji hicho kinakabiliwa na
ukosefu wa sehemu za malisho ya mifugo yao hivyo akaomba Serikali iwapatie maeneo kwa ajili ya
kuchungia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *