
Mashindano ya mchezo wa mpira wa miguu ya Saashisha Cup yaliyoandaliwa na kuratibiwa na Mbunge wa jimbo la Hai Mhe. Saashisha Mafuwe yamekamilika kwa hatua ya kwanza ya mtoano ambapo timu 10 zimeingia hatua ya Robo Fainali.
March 29, 2023 Michezo miwili imepigwa katika viwanja viwili tofauti ambapo mchezo mmoja umezikutanisha timu ya Uswaa FC dhidi ya Harsho FC katika uwanja wa Nkwamwasi, Harsho FC akifanikiwa kuicharaza Uswaa bao moja kwa sifuri.
Mchezo mwingine umewakutanisha Romu Boys dhidi ya Kilimanjaro Teachers katika uwanja wa Half London Boma, Romu Boys wakifyata mkia kwa kipigo cha Bao Mbili kwa Sifuri.

Timu zilizoingia hatua ya Robo fainali ni Home Boys, Rundugai, Kware, Harsho, Masama FC, Machame City, Lambo, Orori, Maili sita na Kilimanjaro Teachers.
Kwa upande wake Captain wa Timu ya Harsho FC Bwn. Richard ameonyesha kuwa na bashasha kwa timu yao kufanikiwa kuingia hatua ya Robo Fainali huku akiahidi kujipanga vizuri kwa Mechi zitakazofuata huku Mwenyekiti wa timu ya Uswaa FC akizitakia kila la heri timu zote zitakazoendelea katika hatua hiyo ya Robo Fainali.
Kasbeth Mushi ambaye ni katibu wa Chama Cha Soka Wilaya ya Hai ambaye amesimamia Michuano hiyo ya Saashisha Cup amemshukuru Mbunge wa jimbo hilo Mhe. Saaashisha Mafuwe kwa kuanzisha michuano hiyo kwani vijana wana hali ya kuonyesha vipaji vyao huku akiwasisitiza kutumia fursa hiyo adhimu.
Hata Hivyo wachezaji wa timu mbalimbali zilizoshiriki na zinazoendelea kushiriki zimemshukuru Mbunge huyo kwa kuona umuhimu wa kuinua vipaji vyao huku wakiomba michuano hiyo kuendelea hata kwa misimu miwili kwa mwaka.














