“TUNATOA shukrani kwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwani ndani ya miaka miwili ya uongozi wake ameendelea kubuni vyanzo vya mapato kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya barabara za vijijini na mijini ambazo ni muhimu katika kukuza uchumi.”

Hii ni kauli ya Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Samson Kalesi wakati wa kuelezea mafanikio yaliyopatika tangu Rais Samia kuingia madarakani.
Anasema baada ya awamu ya sita kuingia madarakani bajeti ya Mkoa wa Rukwa kupitia fedha za maendeleo, mfuko wa jimbo na bajeti ya tozo za mafuta iliongezeka zaidi ya mara mbili ya bajeti ya awali.
Mhandisi Kalesi anasema hadi kufikia mwaka wa fedha 2020/2021 ukomo wa bajeti ya Mkoa wa Rukwa wenye majimbo tano ya uchaguzi ulikuwa ni takribani Sh bilioni 4.28.

“Kwa bajeti hii Mkoa haukuwa na uwezo wa kuongeza mtandao wa barabara kwa maana ya kufungua barabara mpya ambazo zilihitajika kuongeza mtandao wa barabara.”
“Bajeti hii ilikuwa inafanya matengenezo ya kawaida, sehemu korofi na muda maalum ili kuzuia uharibifu na kufanya barabara ziendelee kupitika,” anasema.
Anasema kuwa kwa mwaka 2021/22 TARURA Mkoa wa Rukwa ilitengewa bajeti ya Sh bilioni 12.78 kwa ajili ya ujenzi, matengenezo na usimamizi hii ikiwa ni baada ya kuongezeka kwa fedha za maendeleo, mfuko wa jimbo na bajeti ya nyongeza ya tozo ya mafuta.

Mhandisi Kalesi anasema katika fedha hizo, fedha za Mfuko wa Barabara zilikuwa Sh bilioni 4.28, huku za Mfuko wa miradi ya Maendeleo ni Sh milioni 710 wakati zile za Mfuko Mkuu wa Serikali (Mfuko wa jimbo) ni Sh bilioni 2.5 na fedha za bajeti ya nyongeza ya tozo ya mafuta ni Sh bilioni 2.5.
“Ongezeko fedha hizi zimewezesha kuongeza mtandao wa barabara kwa kufungua barabara mpya, kubadilisha barabara za changarawe kwenda barabara za lami, barabara za udongo kwenda changarawe na kujenga madaraja na makalavati kulingana na mahitaji,” anasema.

TARURA Mkoa wa Rukwa unahudumia mtandao wa barabara wenye wenye urefu wa jumla ya kilomita 2,304.26, kati ya hizo, km 41.82 ni lami, km. 4.52 za zege km. 847.18 changarawe na km. 1418.66 za udongo Madaraja 77, Kalvati (vivuko vidogovidogo) 2498.00, Boksi Kalvati 218 na Madrifti 558.
Mhandisi Kalesi anasema baada ya bajeti kuongezeka mbali na kuzungua barabara mpia na kupandisha hadhi baadhi ya barabara, pia imewezesha ujenzi wa daraja la Kalambo lenye upana wa mita 80 kwa gharama ya Sh bilioni 5.143 na mkandarasi ameshapatikana.
Anasema mafanikio mengine makubwa yaliyopatikana ni ongezeko la mtandao wa barabara za lami kutoka milomita 1 mwaka 2020/21 mpaka kilomita 3 kwa mwaka 2022/23.
Mhandisi Kalesi alisema kuwa katika kuboresha barabara mkakati uliopo TARURA Mkoa wa Rukwa kuendelea na mazungumzo na Wakurugenzi Watendaji ili kupitia mabaraza ya madiwani halmashauri za Sumbawanga MC, Sumbawanga DC, Nkasi CD na Kalambo DC zitenge fedha zinazotokana na mapato ya ndani kwa ajili ya kuhudumia mtandao wa barabara ili maeneo mengi yaweze kufikika kwa urahisi.
“Hii itasaidia wakulima na mazao kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa kufikia masoko na huduma za kijamii kwa urahisi kutokana na kuimarika kwa mtandao wa barabara.”
Mhandisi Kalesi anatumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa Rais samia kwa kuendelea kubuni vyanzo vya mapato kwa ajilikuimarisha miundombinu ya barabara za wilaya.
“Tunapenda kuishukuru Serikali yetu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kubuni vyanzo vingine vya fedha kwa ajili ya kufanya usanifu, ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara za vijijini na mijini ambazo ni nguzo kubwa katika kukuza uchumi wetu pamoja na utoaji huduma muhimu kwa jamii.”