TFRA YATOA MAFUNZO YA UKAGUZI BANDARI KAVU KWA VITENDO

Baada ya watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kupata elimu ya ukagu zi kwa nadharia kwa siku mbili za Alhamisi na Ijumaa, hatimaye siku ya jumamosi, tarehe 25 Machi, 2023 wakiambatana na wawezeshaji walihitimisha mafunzo hayo kwa vitendo.

Akielezea kinachofanyika katika ofisi za kampuni la ETC cargo baada ya watumishi wa Mamlaka kuwasili, (Senior.Operations officer) Hafidh Sadiki alieleza kuwa, kampuni hiyo inajishughulisha na upokeaji wa mizigo kutoka bandarini na kuhifadhi kwa ajili ya kuitoa kwa wateja, ufungaji wa mbolea katika vifungashio, utengenezaji wa mbolea kwa kuchanganya aina tofautitofauti za mbolea inayofaa kwa kilimo.

Akionesha namna kifungashio cha mbolea kinavyopasa kuonekana, Afisa Udhibiti Ubora wa TFRA Bw. John Sosthenes alielezea kuwa, taarifa muhimu zinazopaswa kuwa kwenye mfuko ni pamoja na Jina la Kampuni, Jina la Mbolea, mahala ilipotengenezwa, tarehe ya kuitengeneza, tarehe uya kuisha matumizi, Batch ngani, pamoja na maelezo ya uhifadhi wa mbolea hiyo.

Aliongeza kuwa, endapo umeagiza shehena ya mbolea iliyopo kwenye vifungashio kama vile mifuko pindi inashushwa ili kukaguliwa bandarini na ikabainika taarifa zinazopaswa kuwepo kwenye mfuko hazipo mzigo huwa unakuwa umekosa sifa sitahiki za kuruhusiwa kwenda sokoni hivyo mbolea hiyo itashikiliwa mpaka pale taarifa hizo muhimu zitakapowekwa kwenye vifungashio hivyo.

Akifafanua uwepo wa Idara ya Bandari Kavu, Meneja uendeshaji wa bandari kavu ETC, Kanyunya Issa alisema, kufuatia uwezo mdogo wa kutunza mizigo kwenye bandari ya Dar Es Salaam mizigo mingine inapelekwa bandari kavu kwa ajili ya kuendelea na taratibu nyingine za kukagua na kuitoa mizigo hiyo.

Amesema, katika ofisi yao wametenga ofisi ndogondogo ambapo ikitokea uhitaji wa taasisi inayojishughulisha na ukaguzi kama vile TFRA, basi wanawasilisha maombi ya kupatiwa chumba cha ofisi na ofisi yao inafanya utaratibu wa kuhakikisha chumba kinapatikana kama kilivyoombwa.

Kanyunya aliongeza kuwa, baada ya mzigo kufikishwa bandari kavu taratibu nyingine zinafuata ikiwa ni pamoja na ukaguzi ambapo containner linafunguliwa na wataalamu kujiridhisha endapo kilichopo kwenye taarifa za mzigo kinaendana na mzigo wenyewe na baadaye kuruhusu mzigo kuchukuliwa na mtu au kampuni husika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *