
Wananchi mkoani Arusha wametakiwa kwenda kutoa ushahidi mahakamani kuhusu matukio ya ukatili wa kijinsia yanayotokea katika maeneo yao baada ya kuripotiwa katika vituo vya Polisi.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Felician Mtahengerwa ameyasema hayo leo Machi 25, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Sekei iliiyopo Jijini Arusha ambao waliojitokeza katika mkutano uliondaliwa na Umoja wa Wanawake wa kata hiyo kwa ajili ya kupinga vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji na ulawiti.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema baadhi ya wananchi wamekua na tabia ya kumaliza kimya kimya matukio ya ukatili baada ya kutokea katika jamii zao kwa kupewa hela ama kuahidiwa zawadi ikiwa wataacha kwenda kutoa ushahidi mahakamani au kuacha kuyaripoti.
Aidha amebainisha kuwa Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kuhusika katika kupanga njama za kukwamisha kesi za ukatili katika Jiji la Arusha.
Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Mkoa wa Arusha Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Happiness Temu amesema kupitia mkutano huo wananchi wamepata elimu juu ya ukatili, aina za ukatili, madhara ya ukatili na umuhimu wa kuwahi kuripoti matukio ya ukatili.

Sambamba na hilo pia amebainisha kuwa ili kumaliza matukio ya ukatili ni lazima jamii yote kuwa na ushirikiano wa pamoja wa kukemea vitendo hivyo badala ya kuliachia jeshi la Polisi pekee.
Nao baadhi ya wanawake wa Kata hiyo wamesema wameamua kuandaa mkutano huo ili kuhamasisha jamii kuungana kwa pamoja kukemea vitendo vya ukatili ambavyo vimekua vikiongezeka.