MAKAMU WA RAIS MAZUNGUMZO NA TBL

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi wa Kampuni hiyo Bw. Leonard Mususa, Mazungumzo yaliofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu Dodoma leo tarehe 22 Machi 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 22 Machi 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi wa Kampuni hiyo Bw. Leonard Mususa, Mazungumzo yaliofanyika
katika Ukumbi wa Benki Kuu Dodoma.
Katika Mazungumzo hayo TBL wameipongeza serikali kwa kuendelea kuiunga mkono kampuni hiyo kwa kuweka sera rafiki zinazopelekea kuchochea uzalishaji na maendeleo ya sekta mbalimbali zinazotegemea uwepo wa kampuni hiyo ikiwemo kilimo.
Kampuni ya TBL inatarajia kuwekeza katika ujenzi wa kiwanda cha uzalishaji Pia Moshi mkoani Kilimanjaro kinachotarajia kugharimu dola za marekani milioni 50.
Mkuu wa Mahusiano ya kimataifa wa Kampuni ya vinywaji ya AB-INBEV ambayo ni kampuni tanzu inayomiliki hisa kubwa za Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Bwana John Blood amesema uhusiano uliopo baina ya serikali ya Tanzania na kampuni ya TBL umeweza kukuza biashara pamoja na kukuza uchumi ambapo mpaka kufikia sasa jumla ya wakulima 5000 wameingia mikataba na kampuni hiyo ya uzalishaji wa mtama, shayiri na zabibu inayowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Kwa Upande wake Makamu Rais Dkt. Philip Mpango amesema serikali inatambua mchango wa TBL katika ukuzaji uchumi wa watu na taifa kwa ujumla kwani inachangia katika masuala ya ajira, ulipaji kodi, kuhifadhi mazingira, kutangaza utalii pamoja na kuendeleza kilimo ikiwemo cha shayiri, mtama na zabibu. Aidha ameipongeza kampuni hiyo kwa kuendelea vema kutekeleza wajibu wa kampuni kwa jamii ikiwemo kuungana na serikali katika kipindi cha janga la Uviko19 kutoa misaada mbalimbali ya kukabiliana na
janaga hilo.
Makamu wa Rais amesema serikali inaunga mkono TBL katika ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha bia Moshi mkoani Kilimanjaro kitakachosaidia kuzalisha ajira 5000 kwa wakulima kupitia mikataba ya moja kwa moja.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi wa Kampuni hiyo Bw. Leonard Mususa (wa tatu kukoka kushoto) mara baada ya Mazungumzo yaliofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu Dodoma leo tarehe 22 Machi 2023.

Pia amesema serikali itaendelea kushughulikia changamoto zinazojitokeza baina yake na Kampuni hiyo ili kuendelea kuleta tija ya kibiashara kwa manufaa ya pande zote.
Aidha Makamu wa Rais ameongeza kwamba serikali imedhamiria kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji na biashara nchini ikiwa tayari imefanya mabadiliko ya kisera na kitaasisi kuhakikisha taifa linakua kitovu cha uwekezaji na biashara kwa manufaa ya pande zote mbili.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa kampuni hiyo kuunga mkono programu maalum ya kilimo ya Building Better Tomorrow (BBT) inayotekelezwa hapa nchini hivi sasa hususani kupitia mikataba ya manunuzi pamoja na mafunzo kwa vijana hao. Pia ameisihi TBL kuitangaza Tanzania kama sehemu sahihi ya uwekezaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *