
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule jana 17 Machi 2023 ameshuhudia utiajia saini wa makubaliano ya awali ya ujenzi wa kiwanda cha saruji ambacho uwekezaji wake ni wa thamani ya Dola Milioni 200.
Makubaliano hayo yamefanyika kati ya kampuni ya Alotab & Block BB na Libyan Petrolium ya Libya ambapo kiwanda hicho kinatarajiwa kujengwa Wilayani Kongwa.
Hafla hiyo imefanyika mbele ya wajumbe wa Baraza la Ushauri Mkoa wa Dodoma jijini Dodoma.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amewahakikishia wawekezaji hao mazingira rafiki ya kutekeleza shughuli zao za uwekezaji na kuwakaribisha kuwekeza zaidi katika ujenzi wa viwanda vingine.

“Nawakaribisha Dodoma, Makao Makuu ya Nchi yetu, fursa za uwekezaji ni nyingi wekezeni zaidi katika Mkoa wetu, tunayo ardhi na malighafi ya kutosha” Senyamule alisisitiza.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt Omary Nkullo amesema katika Wilaya yake ekari 500 zimepimwa katika eneo la Pandambili maalumu kwa ajili ya uwekezaji.
Hatahivyo Bw Anyid Dmjed Rajab wa Kampuni ya Libyan Petrolium ya Libra amesema wataendelea kuwekeza katika maeneo mengine katika Mkoa wa Dodoma kutokana na mazingira rafiki ya uwekezaji na upatikanaji wa malighafi.
