KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YARIDHISHWA NA UJENZI NA MABORESHO BANDARI YA DAR ES SALAAM.

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeridhishwa na utekelezaji na usimamamizi wa mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam, unaotekelezwa na Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania – TPA.

Akiongea na Waandishi wa Habari baada ya ziara ya Kamati yake kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Serikali iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Seleman Kakoso amesema Kamati yake imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa maboresho ya Bandari hiyo.

“ kamati inaendelea kuishukuru Serikali kwa mradi huu wa Upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, kuna mabadiliko makubwa yameonekana. Tunaishauri Serikali, Mradi huu ukamilike kwa muda uliopangwa ili Bandari iweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.” Amesema Mhe. Kakoso.

Mhe. Kakoso pia ametoa Rai kwa Wafanyabiashara kuendelea kuitumia Bandari ya Dar es Salaam kupitisha Shehena zao za Mizigo huku Watumishi wakakimbushwa umuhimu wa kuendelea kuwa Wazalendo, Waadilifu na Waaminifu Katika kutekeleza Majukumu yao.

Akijibu hoja za Wajumbe wa Kamati hii, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Godfrey Kasekenya, amesema Serikali ya awamu ya Sita inaendelea Kutenga fedha kwa ajili ya maboresho ya Bandari Nchini kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya Bandari .

“ Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya Bandari Nchini, na kwa Bandari ya Dar es Salaam, lengo la Serikali ni kuiboresha iwe Bandari Bora Afrika Mashariki na Kati.” Amesema Mhe. Eng. Kasekenya.

Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Elihuruma Lema, amesema Mradi wa kimkakati wa Maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam umefikia asilimia 90 na kazi hiyo itakamilika kwa muda uliopangwa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ipo Katika ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya ujenzi na maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam na mwishoni mwa Juma hili Watatembelea na Kukagua Ujenzi wa Bandari ya Karema iliyopo Mpanda Mkoa wa Katavi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *