
Na. mwandishi wetu Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi mkoani Arusha limefanikiwa kukamata bastola moja aina ya CZ 75 LUGER yenye namba za usajili A487385 pamoja na risasi 71 za bastola iliyokuwa inatumiwa na wahalifu.
Akitoa taarifa hiyo leo Kamanda wa Polisi mkoani humo Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amesema silaha hiyo pamoja na risasi zilipatikana katika nyumba iliyopo huko maeneo ya Ilkyurei, Kata ya Kiranyi, wilaya ya Arumeru na mkoa wa Arusha.
Aidha amebainisha kuwa mafanikio hayo yamepatika kupitia katika operesheni maalumu ya kuwasaka watu wanaojihusisha na uhalifu ambayo bado inaendelea.
ACP Masejo amefafanua kuwa wahalifu hao walikimbia baada ya askari Polisi kukaribia kufika katika nyumba hiyo na wanaendelea kufanya upelelezi ili kuwakamata.
Katika operesheni hiyo kwa nyakati tofauti wamefanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 11 wakiwa na mirungi bunda 528 zenye uzito wa zaidi ya kilogramu 162 ambayo walikuwa wakiisafirisha kwa kutumia vyombo vya moto ikiwemo gari pamoja na pikipiki.

Aidha aliendelea kusema kuwa upelelezi wa matukio hayo bado unaendelea, na utakapokamilika majalada yatapelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi.
Sambamba na hilo Jeshi la Polisi mkoani humo limetoa onyo kwa watu wachache wanaojihusisha na matukio ya uhalifu kuacha mara moja kwani watawachukulia hatua.
Pia linawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kudumisha hali ya usalama katika mkoa huo.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka limefanikiwa kumfikisha mahakamani mtu mmoja aitwaye Julius Raphael Mollel (27) mkazi wa kijiji cha Lashaine wilaya ya Monduli kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa darasa la pili (08) ambaye jina lake limehifadhiwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa hilo.

Kamanda Masejo amebainisha kuwa wanaendelea kukutana na wananchi pamoja na viongozi wa kata, mitaa pamoja na vijiji kwa lengo la kutoa elimu kuhusiana na ukatili wa kijinsia pamoja na masuala ya usalama ikiwemo umuhimu wa kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi katika maeneo yao ili kukomesha matukio ya uhalifu.
Pia wanaendelea kutoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya ukatili kwani hatutamuonea muhali mtu yoyote atakayebainika kujihusisha na makosa ya unyanyasaji.