
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson ameiagiza Serikali kupitia Wizara ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi kuwachukulia hatua watumishi wote walioshiriki kusababisha migogoro ya Ardhi katika Jiji la Dodoma na Mikoa yote kwa ujumla Nchini.
Dkt. Tulia ameyasema hayo Bungeni Februari 2, 2023 wakati akihitimisha mjadala wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na taarifa ya kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2022 ambapo baadhi ya Wabunge walilalamikia kuhusu changamoto nyingi za migogoro ya ardhi inayoendelea Nchini.
Spika amesema sio sahihi kwa Serikali kuwahamisha vituo vya kazi watumishi wanaobainika kufanya dhuruma kwa Wananchi kwakuwa hiyo sio adhabu bali ni kumfanya akazalishe migogoro katika eneo lingine hivyo ni wakati sahihi Viongozi kuangalia upya kuhusu adhabu za kuwapatia watumishi hao.
“Hawa watumishi Kama hawachukuliwi hatua ndio maana migogro inaendelea kuzalishwa sio tu Dodoma na maeneo mengine tunajua changamoto hii ipo na watumishi hawa wengine wapo TAMISEMI na wengine wako ardhi, Watumishi waliozalisha migogoro wachukuliwe hatua na mtakapokuwa mnaleta taarifa Bungeni mtatueleza maamuzi ya Serikali ikiwemo kuwalipa wananchi stahiki zao pamoja na watumishi wangapi wamebainika kushiriki kwenye kuwadhurumu wananchi na hatua mlizochukua kwao” Amesisitiza Dkt. Tulia