MKUU WA MKOA WA MBEYA AIPA MIEZI MIWILI KAMPUNI YA ETDCO KUWA IMEKAMILISHA SEHEMU KUBWA YA MRADI REA III MZUNGUKO WA PILI

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera ametoa miezi miwili kwa uongozi wa kampuni ya ETDCO kuwa imekamilisha Mradi wa kusambaza umeme vijijini wa REA III Mzunguko wa Pili katika wilaya tano za mkoa wa Mbeya.

Wilaya hizo ni pamoja na Chunya, Mbeya Vijijini, Kyela, Mbarali na Rungwe.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya amesema sawa sawa na ratiba yao waliyoiwasilisha ikionyesha kuwa maeneo kadhaa ya wilaya za mkoa huo zitawashwa ndani ya mwezi Februari na Machi, 2023 na kuongeza kuwa atawaelekeza Wakuu wa wilaya tano kujiandaa na zoezi la kuwasha umeme kwenye maeneo husika.

“Mfano mmesema kijiji cha Masebe, Itenya na Mwaya, vitawashwa tarehe 7 Februari, 2023 tarehe hizo nawaelekeza Wakuu wa wilaya wakawashe umeme”. Alisema Mhe. Homera.

Katika kikao hicho, kilichoongozwa na uenyekiti wa Mkuu wa mkoa wa Mbeya, kimefanyika tarehe 27 Januari, 2023 alasiri kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Jijini Mbeya ambapo kampuni ya ETDCO iliwakilishwa na Meneja wa Mradi wa REA II, Mzunguko wa Pili, Mhandisi Mustapha Himba na Mwakilishi wa Menejimenti ya kampuni hiyo Dude Fuime.

Katika taarifa ya awali kwa Mkuu wa mkoa, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu alisema kampuni ya ETDCO imekuwa ikisuasua kwenye utekelezaji na kuongeza kuwa tangu ilipoanza kutekeleza Mradi huo, tarehe 3 Agosti, 2021 ambapo ilitarajiwa kukamilika tarehe 02 Februari, 2023 lakini hadi tarehe 26 Januari, 2023 ilikuwa imetekeleza kwa asilimia 43.67 tu.

Mkurugenzi Olotu, ameongeza kwa tafsiri yake ni kuwa kati ya vijiji 139 vilivyokuwa viunganishwe na huduma ya umeme ni vijiji 19 tu ndivyo vimeunganishwa hadi sasa.

Aidha Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Bwana Florian Haule alisema ili kuhakikisha uongozi wa kampuni ya ETDCO unatekeleza agizo hilo kuanzia sasa, wanatakiwa kuwasilisha nakara za manunuzi ya vifaa (Materials) ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya kwa kila manunuzi watakayofanya kuanzia sasa kwa ajili ya ufuatiliaji.

Wakati huo huo Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Mhe. Homera ameuagiza uongozi wa kampuni ya ETDCO kuanzia sasa kuanza kutoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo, na kusisitiza kuwa taarifa hiyo iwe inafika ofisi kwake ijumaa ya kila wiki.

78.68

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *