
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bi Fatma Mwassa ameelezea kufurahishwa na hatua ya Serikali ya kuanza kwa ujenzi wa mradi wa Bwawa la maji la Kidunda katika Mkoa wa Morogoro unaolenga kumaliza changamoto ya upungufu wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ameeleza hayo wakati wa kikao kazi cha kutambulisha rasmi mradi wa Kidunda mbele ya kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa Serikali imeipa hadhi kubwa mkoa wa Morogoro kuwa hazina ya maji, umeme na chakula na hivyo italeta maendeleo makubwa kwa wananchi wake.
“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta maendeleo katika mkoa wa Morogoro, tunajipanga kutumia fursa zilizopo ambapo sasa mkoa wetu unajipambanua kama kitovu cha huduma za na umeme na kupitia mradi huu Wananchi wataenda kunufaika zaidi na huu mradi kijamii na kiuchumi,” ameeleza Mhe Mwassa.
“Kazi kubwa inayoendelea mbele yetu kwa sasa ni zoezi la kutatua changamoto ya mifugo katika vyanzo vya maji na kuondoa wavamizi ikiwa ni katika kusimamia sheria zilizopo na maelekezo ya viongozi wakuu wa Serikali.

Mheshimiwa Mwassa ameongeza kwa kuitaka DAWASA kutenga eneo la kujenga ofisi maalum kwa ajili ya kuwezesha taasisi za ulinzi kufanya kazi kuanzia katika kipindi cha ujenzi na hata baada ya mradi wa Kidunda kukamilika.
Aliongeza kuwa kazi ya ulinzi wa vyanzo vya maji ni endelevu na itasaidia kutoa uhakika wa ulinzi wa vyanzo vya maji ambavyo vina faida lukuki kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Alisistiza kuwa miradi yote ya kimkakati itaendelea kusimamiwa ili utekelezwe kwa ufanisi.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Kidunda kwa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa Serikali inawekeza kiasi cha Bilioni 329 katika kutekeleza mradi huo.

“Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na kukamilika kwake kutamaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani,” alisema Mhandisi Luhemeja.
“Tumekuja kuomba ushirikiano na uongozi wa Mkoa katika usimamizi wa mradi huu ikiwa ni pamoja na ulinzi wa miundombinu mbalimbali ambayo itatumika katika miradi hii.,” amesema na kuongeza kuwa mradi huu wa kimkakati utahitaji ulinzi wa Miundombinu yake ili utekelezwe ndani ya muda uliokusidiwa.
Mhandisi Luhemeja aliongeza kuwa shughuli mbalimbali zimekwishafanyika kuelekea utekelezaji wa mradi huo ikiwemo ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha mradi, ujenzi wa huduma muhimu za kijamii kama vile Shule na kituo cha afya, ujenzi wa miundombinu ya barabara na upimaji wa viwanja 1000 katika makazi mapya. Ameiahukuru serikali na kuongeza kuwa mradi huo ambao umeandaliwa kaa muda mrefu sasa unakwenda kutekelezwa.
Mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda unatekelezwa na Serikali kupitia DAWASA kwa kipindi cha miaka mitatu, kuanzia mwaka huu 2023 hadi mwaka 2026 na unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi maji kiasi cha lita bilioni 190 za maji.
