MRADI WA MAJI KIGOMA KUKAMILIKA DESEMBA 2022

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ametembelea Mradi wa Kuboresha Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Kigoma. Mradi huu unatumia ziwa Tanganyika kama chanzo cha maji, katika eneo la fukwe ya Amani, Kata ya Bangwe Kigoma.

Mhe. Mahundi amesema hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo inatia matumaini, na amewaagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa mazingira Kigoma (KUWASA) kuhakikisha inafuatilia kwa karibu ujenzi wake kwa mkandarasi ili mradi huo ukamilike mapema ili wananchi wapate huduma.

Amesema nia ya serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na huduma ya majisafi na salama. Aidha, amewahakikishia wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji pamoja na Mji mdogo wa Mwandiga wasiwe na mashaka. Maji ya kutosha yanawafikia muda sio mrefu.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma Mhandisi Mbike Jones amesema mradi huo unatarajia kukamilika Desemba 2022 na utaweza kuhudumia wananchi zaidi ya 280,000 wa Manispaa ya Kigoma Ujiji pamoja na mji mdogo wa Mwandiga.

Amesema kwa sasa mahitaji ya wananchi wa maeneo wanayoyahudumia ni lita za ujazo Milioni 24 kwa siku wakati mradi huo unatarajiwa kuzalisha lita milioni 42 kwa siku. Gharama ya mradi huo inatarajiwa kufikia Euro 16,323,152.67 ambazo ni zaidi ya shilingi za Tanzania Bilioni 42 ikiwa ni ufadhili kutoka Jumuia ya Ulaya (EU).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *