MIRADI YA KIMKAKATI INAYOENDELEA KUTEKELEZWA MKOANI MWANZA KUFUNGUA UTALII WA KANDA YA ZIWA

Miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa na Serikali Mkoani Mwanza inaenda kufungua utalii katika Kanda ya Ziwa kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 16,2022 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) katika ziara ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa alipokuwa akikagua maendeleo ya Ujenzi wa Daraja la Kigongo- Busisi, ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR eneo la Fela na uzinduzi wa jengo la huduma ya macho katika Hospitali ya Bugando.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza na wananchi kuhusu faida za miradi ya kimkakati kukuza utalii wa Kanda ya Ziwa katika ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea eneo la Fela kukagua ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa SGR jijini Mwanza.

Ametaja miradi ya kimkakati itakayosaidia kukuza utalii kuwa ni ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi, ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR katika eneo la Fela, Meli na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza.

“Tunaamini kanda ya ziwa itakuwa ni kitovu mahususi cha utalii nchini” Mhe. Masanja amesisitiza.

Amefafanua kuwa uwepo wa miradi hiyo utarahisisha usafiri kwa watalii wanaotembelea jiji hilo kutoka nchi za jirani na wakati huohuo Wizara inaendelea kupanua wigo wa utalii kupitia utalii wa mikutano na utalii wa majini.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimia viongozi mbalimbali wa Serikali alipowasili katika eneo la ujenzi wa Daraja la Magufuli la Kigongo-Busisi kwa ajili ya kukagua ujenzi wake jijini Mwanza.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masanja amehamasisha wananchi hususan wa mkoa wa Mwanza kuendelea kupanda miti ili kutunza mazingira, kutunza uwepo wa hali ya hewa nzuri na kutunza vyanzo vya maji.

“Wizara ya Maliasili na Utalii ina mkakati wa kuhakikisha kila mwananchi anapanda miti miwili, hivyo imeanzisha vitalu vya miti ambayo itagawiwa kwa wananchi”amesema.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, Mhe. Furaha Matondo wakifurahia jambo wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ya kukagua ujenzi wa Daraja la Magufuli la Kigongo-Busisi jijini Mwanza. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Sengerema , Mhe.Hamis Tabasamu.

Aidha, ameitumia  fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake kwa kufanya kazi kwa nguvu zote kuhakikisha miradi hiyo inasonga mbele.

“Tuko pamoja kuhakikisha Serikali inasonga mbele chini ya Kiongozi wetu Rais Samia Suluhu Hassan” amesema Mhe. Masanja.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akiwa ameongozana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ya kukagua ujenzi wa Daraja la Magufuli la Kigongo-Busisi jijini Mwanza.

Ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa inaendelea Mkoani Mwanza ambapo tarehe 17 Oktoba, 2022 atatembelea Kisiwa cha Ukerewe, Kisiwa cha Gana na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Stendi ya Nyegezi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *