Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) imekuwa chachu ya ongezeko la ukusanyaji wa mapato kupitia vituo jumuishi vya urasimishaji na uendelezaji wa biashara ambavyo imevianzisha katika maeneo mbalimbali nchini.

Mhe. Jenista ameyasema hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kabla ya kuzindua Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara katika Manispaa hiyo akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za MKURABITA mkoani Kilimanjaro.
Mhe. Jenista amesema ongezeko la ukusanyaji wa mapato kupitia vituo hivyo jumuishi linajidhihirisha wazi kwenye Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara kilichop Halmashauri ya Manispaa ya Moshi baada ya makusanyo ya robo mwaka kuongezeka kwa shilingi 71,336,000.

“Kupitia kituo hiki jumuishi cha Manispaa ya Moshi, Serikali imeboresha ukusanyaji wa mapato yanayotokana na ada za leseni za biashara kwani wastani wa makusanyo ya ada hiyo kabla ya kituo hiki kuanzishwa ilikuwa shilingi140,624,000 kwa robo mwaka lakini baada ya uwepo wa kituo hicho wastani wa makusanyo umeongezeka na kufikia shilingi 212,000,000 ambalo ni ongezeko la shilingi 71,376,000.
Mhe. Jenista ameipongeza Halmashauri ya Manipaa ya Moshi kwa ongezeko hilo la ukusanyaji wa mapato kupitia kituo hicho jumuishi kwani imeitikia wito wa Serikali wa kubuni vyanzo mbalimbali vya ukusanyaji mapato kwa maendeleo ya taifa.

Aidha, Mhe. Jenista ameongeza kuwa, urasimishaji umeongeza wigo wa walipa kodi kwa kuingiza biashara ndogondogo za waendesha bodaboda na bajaji zilizorasimishwa katika mfumo rasmi wa walipa kodi nchini.
Akielezea faida ya uanzishwaji wa Vituo Jumuishi vya Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara, Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), CPA. Dkt. Seraphia Mgembe amesema kupitia kituo jumuishi cha Manispaa ya Moshi, Serikali imefanikiwa kusajili walipa kodi ambao hapo awali walikuwa wakiogopa kusajiliwa kwa kutokuona umuhimu wake.

Amesema zamani kodi ilikuwa haitamkwi hadharani lakini sasa hivi inatamkwa kwani kila mmoja amepata ufahamu wa kuchangia pato la taifa kwa maendeleo.
“Baada ya kuwasajili kwenye kwenye mfumo, wanatambua umuhimu wa kulipa kodi na sasa wanaendelea kulipa, kutoa ada za leseni na wanafanya biashara zao kwa kujiamini,” CPA Dkt. Seraphia ameongeza.
Mhe. Jenista amefanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Kilimanjaro yenye lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za MKURABITA na kuzungumza na watumishi wa mkoa huo ili kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.

