TANZANIA YAPIGA KURA YA KUTOKUEGEMEA UPANDE AZIMIO LA UN KUPINGA MIKOA YA UKRAINE KUCHUKULIWA NA URUSI

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura kuunga mkono azimio linalolaani hatua ya Urusi kuyanyakua maeneo ya kusini na mashariki mwa Ukraine.

Nchi 143 zimeunga mkono azimio hilo, huku tano tu zikilipinga ikiwemo Urusi yenyewe, Korea Kaskazini na Belarus.

Nchi nyingine 35, zikiwemo Tanzania, China, India, Pakistan na Afrika Kusini zimepiga kura ya kutofungamana na upande wowote.

Awali Urusi ilishindwa katika juhudi zake za kutaka kura hii ipigwe kwa siri, kabla ya kura hiyo kupigwa, Marekani ilifanya jitihada kubwa za kidiplomasia kuzishawishi Afrika Kusini na India ziunge mkono azimio hilo lakini haikufanikiwa.

China ambayo ni Mshirika wa kimkakati wa Urusi, imesema kura hiyo ilikuwa na sura ya vita baridi na haina tija lakini Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas Greenfield amesema inapeleka ujumbe kwamba Dunia haitavumilia tabia ya nchi moja kuyachukua kwa nguvu maeneo ya Majirani zake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *