UJENZI WA MABWAWA KUSAIDIA KUONDOA CHANGAMOTO YA MAJI DODOMA

Bodi ya Taifa ya Maji imefanya ziara ya kutembelea miradi ya ujenzi wa bwawa la maji la Mtamba Wilayani Mpwapwa na Bwawa la Manda wilayani Chamwino mkoani Dodoma ambayo kwa pamoja yanayotarajia kugharimu shilingi Bilioni 1.3. Mabwawa haya yanajengwa na Bodi ya Maji ya Bonde la Rufiji na yanatarajia kutumika katika shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo cha umwagiliaji, mifugo na matumizi ya kawaida ya binadamu.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Mbogo Futakamba, amesema mabadiliko ya tabia nchi yameathili sehemu mbalimbali nchini hivyo uamuzi wa kujenga miundombinu ya kuvuna maji ya mvua itasaidia wananchi kuwa na uhakika wa usalama wa chakula, mazingira, nishati na afya. Ameipongeza serikali na kuitaka ihakikishe mabwawa hayo yanakamilika ndani ya wakati. Aidha wahakikishe wanaweka alama za mipaka ili kuzuia shughuli za kibinadamu ambazo zinaweza kuathili uendelevu wa mabwawa hayo.

Awali akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa mabwawa hayo Mhandisi Geofrey Semkonda wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji amesema mabwawa yote mawili yanatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi wa 10 mwaka huu na yatatatua changamoto ya huduma ya maji kwa wananchi na mifugo inayozunguka maeneo hayo. Amesema ujenzi wake umezingatia mahitaji ya wananchi kwa sasa na baadaye katika maeneo yanayozunguka mabwawa hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulika na Uhifadhi na Utunzaji Vyanzo vya Maji Wizara ya Maji, Rosemary Rwebugisa Amesema Mabwawa yanayojengwa ni sehemu ya mkakati wa Wizara kuhakikisha rasilimali mvua inatumika kama chanzo cha maji ili kuhudumia maeneo ambayo hayana vyanzo vingine vya maji, Lengo ni kuhakikisha kila mtanzania anafikiwa na huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *