Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro ametoa ufafanuzi juu ya Sintofahamu kuhusiana na Matokeo ya Taasisiya Mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo Tanzania LST, kufuatia Mjadala ulioibuka katika sehemu mbalimbali kwamba kwanini wanafunzi hao wanafeli sana.
Akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma Dkt Ndumbaro amesema mjadala huo si mpya, ni wa muda mrefu kwani historia ya wanafunzi wachache kufaulu mitihani ya Taasisi hii haijaanza leo ni ya siku nyingi licha ya kwamba hailengi kumkomesha mtu yoyote bali inalenga kuweka viwango vya juu.

Ameeleza kuwa Vinawekwa viwango vya juu kwa sababu Sheria ni jambo muhimu katika utawala bora, utawala wa Sheria, kuleta amani na utulivu pamoja na utoaji wa haki, hivyo ni lazima wawe na imani na wanasheria tunaowapa jukumu hilo.
“Vinawekwa viwango vya juu kwa sababu Sheria ni jambo muhimu katika utawala bora, utawala wa Sheria, kuleta amani na utulivu pamoja na utoaji wa haki, hivyo ni lazima tuwe na imani na wanasheria tunaowapa jukumu hilo” Alisema Dkt. Damas Ndumbaro

Ametaja Takwimu za ufaulu wa mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo Tanzania huku waliofeli kufikia asilimia 19 kati ya asilimia 100 ambayo ni asilimia ndogo na inatokea kokote duniani hivyo kama kuna mwanafunzi anayehisi ameonewa, kuna mfumo wa kukata rufaa ambao upo na unafanya kazi.
“Tangu Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania imeanzishwa, wanafunzi 8,255 kati ya wanafunzi 13,974 wamefaulu sawa na asilimia 59.074 na wanafunzi waliofeli baadhi ya masomo ambao wanaruhusiwa kurudia masomo hayo ni asilimia 21.619” Alisema Dkt. Damas Ndumbaro
“Takwimu zinaonesha kuwa, asilimia kubwa ya wanaorudia baadhi ya masomo waliyofeli huwa wanafaulu, hivyo ufaulu kwa ujumla utakuwa kwenye asilimia 81, Kwa takwimu hizi za ufaulu, asilimia ya waliofeli kabisa ni asilimia 19 kati ya asilimia 100 ambayo ni asilimia ndogo na inatokea kokote duniani” Alisema Dkt. Damas Ndumbaro

Kufuatia Mijadala hiyo, Serikali imeunda Kamati ya watu saba ambayo imepewa siku 30 kuleta taarifa juu ya tuhuma hizi ambapo amesema Kamati hii haijahusisha Waalimu wala Mstaafu yeyote wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), wala Walimu kutoka Vyuo vinavyotoa elimu ya sheria, bali wamehusisha wadau wengine ili walete majibu ya ukweli na yenye tija.
“Serikali imeunda Kamati ya watu saba ambayo imepewa siku 30 kuleta taarifa juu ya tuhuma hizi. Kamati hii haijahusisha Waalimu wala Mstaafu yeyote wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST) wala Walimu kutoka Vyuo vinavyotoa elimu ya sheria, tumehusisha wadau wengine ili walete majibu ya ukweli na yenye tija” Alisema Dkt. Damas Ndumbaro