BARABARA YA KIDATU-IFAKARA KUKAMILIKA MEI

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amemtaka Mkandarasi Reynolds Construction Company Nigeria ltd, anayejenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kidatu-Ifakara yenye urefu wa KM 66.9 pamoja na daraja la Ruaha Mkuu lenye urefu wa mita 130, kuhakikisha ujenzi huo unakamilika mwezi Mei mwakani.

Amesema changamoto zote zilizokuwa zikichelewesha mradi huo zimepatiwa ufumbuzi hivyo kazi iliyobaki ni kwa Mkandarasi kukamilisha ujenzi.

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya akifafanua jambo kwa wakazi wa Mang’ula (hawapo pichani), alipokagua ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara KM 66.9 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Morogoro.


Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi huo Eng. Kasekenya amesema barabara hiyo itakuza kilimo katika mkoa wa Morogoro na ukanda wa kusini mwa Tanzania, kupunguza muda wa usafiri na gharama
za kusafirisha mazao na pembejeo za kilimo, kuongeza thamani ya mazao na hivyo kukuza uchumi wa wananchi kwa ujumla.


“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunaufungua mkoa wa Morogoro ambao ni ghala la chakula ili kuunganisha kwa njia fupi na mikoa ya Njombe na Ruvuma,” amesema Naibu Waziri huyo.

Muonekano wa barabara ya Kidatu-Ifakara KM 66.9 katika hatua mbalimbali ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoaniMorogoro.


Amemtaka msimamizi wa mradi huo, Kitengo cha Uhandisi Ushauri cha TANROADS (TECU), kuhakikisha maeneo yote yanayohitaji kuboreshwa ilikuimarisha usalama katika barabara hiyo yanafanyiwa kazi haraka na kwa viwango.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Eng. Lazack Kyamba amesema mradi huo ambao umefikia asilimia 68 uko katika hatua nzuri na watamsimamia mkandarasi ili ukamilike kama ilivyopangwa.


Barabara ya Kidatu-Ifakara KM 66.9 ni sehemu ya barabara ya Mikumi-Ifakara yenye urefu wa KM 130 inayopita katika ukanda wenye uzalishaji mkubwa wa mazao hivyo kukamilika kwake kutaboresha ustawi wa jamii kwa kukuza uchumi wa watu na taifa kwa ujumla.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro Eng. Lazack Kyamba akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi Eng.
Godfrey Kasekenya alipokagua ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara KM 66.9 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani
Morogoro.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya amekagua na kuridhishwa na ujenzi wa barabara ya Dumila –Kilosa- Mikumi KM 142, sehemu ya Rudewa-Kilosa KM 24 ambayo inajengwa na wakandarasi wazawa na
kuwataka waongeze bidii ili kujenga imani kwa Serikali.


Kampuni hiyo ya Umoja-Kilosa JV inajumuisha kampuni saba za kihandisi za wazawa ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuwajengea uwezo wakandarasi wazawa ili kumudu kujenga miradi mikubwa na hivyo kunufaika kiuchumi na kiuzoefu.


“Barabara hii ya Dumila-Kilosa-Mikumi inayopita nje ya mbuga ya wanyama ya mikumi itakapokamilika itapunguza msongamano wa magari katika barabara ya Morogoro-Iringa na kupunguza ajali za magari kugonga wanyama katika mbuga hiyo,” amesema Eng. Kasekenya.

Msimamizi wa ujenzi wa barabara ya Rudewa-Kilosa KM 24 Eng. Protas
Mwasyoke akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey
Kasekenya alipokagua ujenzi wa barabara hiyo ambayo ujenzi wake kwa
kiwango cha lami unaendelea mkoani Morogoro.

Msimamizi wa mradi huo Eng. Protas Mwasyoke amesema wamejipanga kuhakikisha sehemu iliyobaki ya kuunganisha kwa lami barabara ya Dumila-Rudewa –Kilosa inakamilika ifikapo Machi mwakani.


Naibu Waziri Kasekenya yuko katika ziara ya siku tatu mkoani Morogoro kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara za lami.

Muonekano wa barabara ya Rudewa-Kilosa KM 24, ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Morogoro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *