WAZIRI MKENDA AAGIZA KUONGEZWA KWA PROGRAMU ZA MADINI VETA GEITA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda ameagiza kuongezwa kwa programu za madini katika Chuo cha Ufundi na Mafunzo Stadi cha Mkoa wa Geita ili kuwezesha vijana wanaofanya shughuli za madini kupata ujuzi

Prof. Mkenda ametoa maagizo hayo Oktoba 10, 2022 Mkoani Geita alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho ambapo amesema chuo hicho hakitakuwa na tija kama hakitatoa mafunzo hayo kwa kuwa shughuli kubwa za kiuchumi mkoani humo ni za madini.

Ameongeza kuwa hata mabadiliko ya mitaala yanalenga kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanawaandaa vijana kufanya kazi popote duniani na pia kuwawezesha kumudu mazingira yanayowazunguka pamoja na kupata ujuzi wa shughuli za kiuchumi zilizopo katika eneo wanaloishi.

“Ukiangalia maudhui ya programu zitakazokuwa hapa hakuna masuala ya madini na ukweli Geita ni Mkoa wa madini kuna migodi mikubwa mpaka ya watu binafsi hivyo hatuwezi kuwa na chuo cha ufundi hapa alafu hakina karakana ya kutoa mafunzo ya madini, hivyo naelekeza kuandaliwa kwa programu pamoja na karakana za kutoa mafunzo hayo ili kuwezesha vijana kuwa na umahiri katika kufanya shughuli zao za madini” amesisitiza Waziri Mkenda.

Kiongizi huyo ameongeza kuwa Canada ilishaonyesha nia ya makampuni yake ya madini kutaka kufanya kazi na taasisi za elimu ili ziweze kutoa mafunzo kwa ajili ya kuandaa wataalamu watakaokuwa na ujuzi katika sekta ya madini.

Ameendelea kueleza kuwa watawasiliana na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ili kuona namna kushirikisha makampuni ya madini kutoa ushauri juu ya mafunzo na mitaala inayofaa.

Nae msimamizi wa mradi huo kutoka Chuo cha Ufundi Arusha ATC Msanifu Majengo Richard Idelya ameleeza kuwa ujenzi umefikia asilimia 94 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Mwezi Novemba Mwaka huu na kukabidhiwa.

Huku Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa VETA Anthony Kasore akieleza kuwa Chuo hicho kinatarajiwa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1,240 kwa programu za muda mfupi na mrefu katika fani mbalimbali na kwamba kitakapokamilika kitakuwa kimegharimu zaidi ya shilingi bilioni sita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *