NAIBU WAZIRI WA KILIMO ATEMBELEA MRADI WA UCHIMBAJI WA VISIMA NZUGUNI DODOMA

NAIBU Waziri wa Kilimo na Mbunge Dodoma wa Mjini, Anthony Mavunde, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa kuweza kushirikiana na wananchi katika kutatua kero ya maji licha ya changamoto zote zilizopo.

Ameyasema hayo jana wakati wa ziara yake katika eneo la Nzuguni ambapo visima vitano vimechimbwa katika eneo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabiri Shekimweri (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph wakionja maji kwenye zoezi la upimaji maji katika moja ya visima vitano vilivyochimbwa na DUWASA eneo la Nzuguni jijini Dodoma wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo hilo jana.

“Ninampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutatua changamoto ya upungufu wa maji katika jiji la Dodoma, tunamshukuru Rais kwa mipango ya muda mrefu ya kati na mipango ya muda mfupi ya kutatua changamoto hii.” Alisema Mavunde

Alisema yeye kama Mbunge ataendelea kuishauri serikali namna nzuri ya kupata maji kabla ya utekelezaji wa miradi mikubwa kuanza na kuweka fedha katika uchimbaji wa visima virefu pembezoni ili tuweze kupata maji ya uhakika.

NAIBU Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Dodoma, Anthony Mavunde (kulia), Mkuu  wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabiri Shekimweri (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph wakiangalia jenereta linalotumika katika zoezi la upimaji maji moja ya visima vitano vilivyochimbwa na DUWASA, Nzuguni jijini Dodoma wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo hilo jana.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa majisafi Nzuguni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph alisema zaidi ya wakazi 37,000 waishio katika ukanda wa Nzuguni jijini Dodoma wanatarajia kunufaika na mradi wa maji baada ya kubainika uwepo wa bonde lenye maji mengi katika eneo la hilo.

“Maeneo ambayo utafiti na uchimbaji visima unaendelea yanamilikiwa na wananchi na mara baada ya kukamilika kazi hizo zoezi la uthamini litafanyika kwa ajili ya kulipa fidia ili kuyatwaa kwa matumizi ya mamlaka.”

NAIBU Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Dodoma, Anthony Mavunde (wa tatu kulia), Mkuu  wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabiri Shekimweri (wa pili kulia) wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph akiwaonyesha ramani ya tanki la maji litakapojengwa kwa ajili ya visima vitano vilivyochimbwa na DUWASA, Nzuguni jijini Dodoma wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo katika eneo hilo jana.

Alibainisha kuwa mradi huo utaongeza uzalishaji wa majisafi kutoka wastani wa lita milioni 67.8 hadi lita milioni 75.5 kwa siku sawa na ongezeko la asilimia 11.4 ya uzalishaji wa sasa.

Aidha, utaondoa mgao wa maji maeneo ya Nzuguni, Ilazo na Kisasa na utawezesha maji yanayohudumia ukanda huo kupelekwa maeneo mengine ya Jiji.

“Ongezeko hili litaongeza asilimia 11.7 ya mahitaji ya sasa ya jiji lote la Dodoma ambayo ni lita milioni 133.8 kwa siku,”alisema.

Watoto wakichota maji kwenye zoezi la upimaji maji katika moja ya visima vitano vilivyochimbwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) katika eneo la Nzuguni jijini Dodoma jana.

“DUWASA tunaishukuru Wizara ya Maji kwa kuwa tayari kutenga fedha za kutekeleza mradi huu kwa haraka na kupunguza adha ya maji katika maeneo husika, kipindi miradi mikubwa ya Farkwa na Mtera ikiendelea kutekelezwa,”alieleza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Jabir Shekimweri aliipongeza DUWASA kwa hatua hiyo huku akiishauri kuendelea na kasi ili kupata maji maeneo mengine.

NAIBU Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Dodoma. Anthony Mavunde, akionja maji kwenye zoezi la upimaji maji katika moja ya visima vitano vilivyochimbwa na DUWASA eneo la Nzuguni jijini Dodoma wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo hilo jana. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabiri Shekimweri na wa pili kushoto Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph wakionja

Aidha, alishauri wananchi wanaopisha miradi hiyo kulipwa fedha zao mapema ili eneo libaki kuwa chanzo cha maji na wanaojenga wajulishwe kuhusu kuzingatia suala la upandaji miti ili kutunza mazingira.

Pia, aliishauri DUWASA kuzingatia afya ya walaji kwa kuhakikisha mkondo wa maji hauingiliani na mfumo wa majitaka.

MKUU wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabiri Shekimweri akionja maji kwenye zoezi la upimaji maji katika moja ya visima vitano vilivyochimbwa na DUWASA. Nzuguni jijini Dodoma wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo hilo jana. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph na Naibu Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Dodoma, Anthony Mavunde.

Diwani  wa Kata ya Nzuguni Aloyce Luhega alishauri mamlaka hiyo kuangalia uwezekano wa kupeleka maji katika eneo la Mahomanyika ambalo lipo kwenye kata hiyo lenye changamoto kubwa ya maji.

DUWASA kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Maji wamechimba visima vitano katika eneo la Nzuguni kupitia mradi huo utakaogharimu zaidi ya sh. bilioni 4.8 maji yatafikishwa kwa wakazi wa Nzuguni, Ilazo, Swaswa na Kisasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *