VITENDO VYA UKATILI HAVIVUMILIKI-WAZIRI GWAJIMA Na WAJJWM,

Dar es salaam

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Serikali haitavumilia vitendo vya ukatili vinavyoendelea kutokea kwenye jamii.

Waziri Gwajima ameyasema hayo tarehe 07 Oktoba, akiwa katika ziara yake Jijini Dar es salaam, kata ya Kivule alipomtembelea Mtoto Daudi Mabwega mwenye umri wa miaka minne aliyefanyiwa ukatili na baba yake mzazi wa kuchomwa ya maji ya moto mkononi kwa kosa la kula mboga bila idhini ya mzazi huyo.

Amesema Jamii inatakiwa kuwatunza watoto kwani ni hazina kwa Taifa hivyo wanapaswa kulindwa kwa hali yoyote na akiwa ni Waziri mwenye dhamana ya watoto atahakikisha haki zao zinalindwa.

“Mzazi ni mtu wa kwanza anayetakiwa kuwa Faraja kwa Mtoto wake aliyemzaa, hatuwezi kuendelea kuvumilia kuona Wazazi ambao badala ya kuwa viongozi wanawakatili hawa watoto, Serikali itamfikia kila mzazi, mlezi na mwanajamii aliyefanya ukatili kwa mwanajamii mwingine hususani watoto” amesema Mhe. Gwajima.

Kwa upande wake Afisa Utawi wa Jamii, hospitali ya Wilaya ya Kivule Irene Shembelu aliyeibua ukatili huo amesema Mtoto huyo alifanyiwa ukatili na baba yake baada ya migogoro ya kifamilia iliyosababisha mama wa mtoto kuondoka na kuwaacha watoto na baba yao pekee.

“Tuliipokea kesi ya Mtoto huyu kuwa amekatiliwa na baba yake mzazi kwa kosa la kula maharage waliyotegemea kula baada ya baba kurudi, kwani watoto hawa wanajilea wenyewe, baba akitoa asubuhi anarudi usiku” Alisema Irene Shembelu.

Kwa upande wake Inspekta Mdasi Lukato akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Dawati la Jinsia Kanda Maalum ya Polisi Dar es salaam amesema hatua kali zitachukuliwa kwa kitendo kilichofanyika na baba huyo.

Naye mlezi aliyeaminiwa kumlea Mtoto Daudi na ndugu zake Bi. Zahra Omary (fit person) amesema alimpokea Mtoto huyo mwezi Agosti mwaka huu kutoka kwa Afisa Ustawi wa Jamii akiwa na Hali mbaya.

Baadhi ya wananchi wakizungumza katika mkutano wa hadhara wamemshukuru Mhe. Gwajima kwa kuwatembelea na kujua changamoto zao kwani vitendo vya ukatili katika kata hiyo ni vingi lakini wanajamii wanakabiliana navyo kwa jitihada mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *