MHE JENISTA AWATAKA WAJUMBE WA BARAZA KUU LA WAFANYAKAZI KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO YA WATUMISHI NA WANANCHI KWA WAKATI KATIKA MAENEO YAO YA KAZI KAMA AMBAVYO SERIKALI IMEKUSUDIA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka wajumbe wa Mkutano wa Tatu wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi Tanzania Bara kuhakikisha wanashughulikia kwa wakati malalamiko ya watumishi wa umma na wananchi katika maeneo yako ya kazi kama serikali ilivyokusudia, ili kuwapunguzia gharama za kusafiri hadi Makao Makuu ya nchi jijini Dodoma kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa masuala yao ya kiutumishi.

Mhe. Jenista ametoa wito huo kwa wajumbe wa baraza hilo, wakati akifungua Mkutano wa Tatu wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi Tanzania Bara unaofanyika mjini Morogoro.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Wajumbe wa Mkutano wa Tatu wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi Tanzania Bara wakati akifungua mkutano wa baraza hilo mjini Morogoro.

“Wajumbe wa baraza, mnaposhughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi mhakikishe mnayashughulikia kwa wakati ili kuwaondolea mzigo wa gharama katika kutafuta ufumbuzi kwa viongozi na waajiri kwenye ngazi ya kitaifa,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikisisitiza umuhimu wa watendaji kushughulikia malalamiko ya watumishi wa umma ili kuwajengea ari na morali ya kutoa huduma bora kwa wananchi, hivyo wajumbe wa baraza hawana budi kuunga mkono jitihada za serikali kuhimiza ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi wa umma na wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na taasisi za umma nchini.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma akieleza ajenda kuu ya Mkutano wa Tatu wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi Tanzania Bara kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) kabla ya Waziri huyo kufungua mkutano wa baraza hilo unaofanyika Mjini Morogoro.

Katika kutoa msisitizo wa ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi na watumishi wa umma, Mhe. Jenista ametoa wito kwa waajiri kuutumia ipasavyo mfumo wa e-Mrejesho katika kushughulikia malalamiko ili kupata mrejesho utakaotumiwa na serikali kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma, Bi. Jane Mihanji amesema, baraza litatoa kipaumbele cha matumizi ya e-Mrejesho serikalini ili kuendana na kasi ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo inakua kwa kasi kubwa.

Wajumbe wa Mkutano wa Tatu wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi Tanzania Bara wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati akifungua mkutano wa baraza hilo mjini Morogoro.
 

Akizungumzia uwajibikaji kwa wajumbe wa baraza, Bi. Mihanji amesema kuwa wao kama viongozi na wawakilishi wa watumishi wa umma watahakikisha wanawakumbusha watumishi kutekeleza wajibu wao ipasavyo, ili wawe na uhalali wa kudai haki na stahili zao pindi wanapozikosa kutokana na sababu mbalimbali.

Katibu wa Mkutano wa Tatu wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi Tanzania Bara, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Bi. Agness Meena akitoa neno la utangulizi kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) kuzungumza na wajumbe wa baraza hilo linalofanya mkutano wake Mjini Morogoro.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema wajumbe wa baraza watashiriki katika kutekeleza ajenda kuu moja ya msingi ya kupitia na kuridhia miundo ya maendeleo ya utumishi ya kada zilizo chini ya wizara mbalimbali katika Utumishi wa Umma ili kuendana na mahitaji ya watumishi wa umma nchini.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa A. Mussa akitoa salamu za Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) kabla ya waziri huyo kufungua Mkutano wa Tatu wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi Tanzania Bara unaofanyika Mjini Morogoro

Mkutano huo unaoratibiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, unafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 06 hadi 08 Oktoba, 2022.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma, Bi. Jane Mihanji akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wajumbe wa baraza hilo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (huyupo pichani) mara baada ya Waziri huyo kufungua Mkutano wa Tatu wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi Tanzania Bara unaofanyika Mjini Morogoro
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Mkutano wa Tatu wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi Tanzania Bara unaofanyika Mjini Morogoro. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi na kulia kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *