MCHANGO WA WACHIMBAJI WADOGO WAIMARIKA 30%- MHANDISI SAMAMBA

Serikali kupitia Wizara ya Madini hapa Nchini imedhamiria kuboresha na kuimarisha mazingira ya utendaji kazi, kuvutia wawekezaji, kuimarisha usimamizi wa sekta na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na madini.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji Wa Tume Ya Madini Mhandisi Yahya Samamba wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Octoba 7, 2022 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji na vipaumbele vya Taasisi kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo amesema miongoni mwa vipaumbele walivyonavyo ni uboreshwaji na na uimarishwaji katika sekta ya madini ikiwemo kuimarisha usalama na mazingira ya kufanyia kazi.
“Kuimarisha usalama, afya, mazingira na uzalishaji katika migodi, kuwezesha mazingira ya wananchi kunufaika na rasilimali madini, kuelimisha umma, kuboresha mawasiliano, kuendeleza rasilimali watu na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, Kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kutoka sekta ya madini kiliongezeka kutoka Shilingi bilioni 346.275 mwaka 2018/19 hadi Shilingi bilioni 624.61 mwaka 2021/22 sawa na ongezeko la 44.5%.”


Mhandisi huyo ametanabaisha kiwango cha ajira kufikia hatua 97% ikilinganishwa na mwaka 2018 ambapo watanzania wameendelea kupata ujuzi huku zaidi ya shilingi Bilioni 29.8 zikiwa zimetumika kutoa huduma kwa jamii zinazoizunguka miradi ya madini.
“Ajira kwa wazawa imefikia 97% ikilinganishwa na chini ya 70% mwaka 2018. Kupitia ajira hizo, Watanzania wameendelea kupata ujuzi na uzoefu ili baadae miradi hii isimamiwe na Watanzania kwa 100%, Pia zaidi ya Shilingi bilioni 29.8 zimetumika kwa ajili kutoa huduma kwa jamii zinazoizunguka miradi ya madini kwa kipindi cha kati ya mwaka 2019 hadi 2021.”
“Mwaka 2021, mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa ulikuwa 7.3 % kutoka 4.8% mwaka 2018. Lengo likiwa kufikia 10% ifikapo 2025, Ukuaji wa sekta ya madini mwaka 2021 ulikua kwa 9.6% ukilinganisha na ukuaji wa 1.5% mwaka 2018. Aidha, jumla ya mitambo mitatu ya kusafishia dhahabu imejengwa na mashine 23 za kuongeza thamani madini zimekamilika.


Aidha mchango wa wachimbaji wadogo imeimarika kwa kufikia asilimia 30% na tume imejipanga kusimamia miradi yote ya madini itakayozalisha nishati safi na jumla ya leseni 3 za uchimbaji mkubwa zimetolewa kati ya mwaka 2020-22 kwa lengo la uwekezaji wenye tija.
“Mchango wa wachimbaji wadogo kwenye mapato yanayokusanywa na Tume umeimarika hadi kufikia 30% mwaka 2021 ikilinganishwa na chini ya 24% mwaka 2018. Jumla ya leseni 3 za uchimbaji mkubwa zimetolewa kati ya mwaka 2020 – 2022, uwekezaji huu una mtaji wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 100, hivyo kuimarisha uchumi wa nchi na kutoa fursa za ajira.


Amehitimisha kwa kusema katika bajeti ya mwaka 2022/2023 ameeleza miongoni mwa vipaumbele vilivyopo ni pamoja na kukusanya shilingi Bilioni 822, sambamba na kufuta leseni zote ambazo haziendelezwi, kusimamia ipasavyo miradi ya madini, kuimarisha zaidi hali ya usalama, afya na mazingira ya migodi sambamba na kusimamia ushiriki wa wazawa.
“Kuendelea kufungamanisha sekta ya madini na sekta zingine, kusimamia ipasavyo ushiriki wa wazawa, kuendelea kuvutia wawekezaji, kuzuia kupambana na utoroshaji na biashara haramu ya madini na kuendelea kutoa elimu kwa umma na wawekezaji”
kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kuna haja ya kushirikiana na sekta binafsi kutafiti kufahamu yaliyopo ili yawezekunufaisha nchi kwani nchi yetu ni miongoni mwa nchi zenye utajiri mkubwa wa madini .
“Nchi yetu ni moja ya nchi ambazo zimejaaliwa na Mungu kuwa na utajiri mkubwa wa madini, tunachokifanya ni kutafiti kufahamu yalipo ili yaweze kunufaisha nchi, katika kutekeleza hili tunashirikiana na sekta binafsi. Tunataka tufanye utafiti wa kina kujua madini mengi zaidi angalau kufikia 40% ili Serikali ijenge mazingira mazuri na kuzihamasisha sekta binafsi kuchimba madini hayo”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *