WATU WENYE ULEMAVU WAPONGEZA JITIHADA ZA SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO ZAO.

Na: Mwandishi Wetu – Dodoma

WATU Wenye ulemavu wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza kasi ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Pongezi hizo zilitolewa jijini Dodoma, mbele ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Pro. Jamal Katundu wakati akipokea vifaa vya watu wenye ulemavu kutoka Taasisi ya ASA Microfinance.

Katibu Mkuu,Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Prof. Jamal Adam Katundu (katikati), pamoja na Abu Sayed Mkurugenzi wa Taasisi ya ASA Microfinance Tanzania Limited (kushoto), wakimkabidhi Mwenyekiti wa Shirika la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Mkoa Wa Dodoma Ommary Lubuva (kulia) kiti mwendo (wheelchair) wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu iliyofanyika katika ofisi hiyo mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Oktoba 6, 2022.

Amesema vifaa vilivyopokelewa ni viti mwendo pisi 35, mafuta maalumu kwa ajili ya watu wenye ualbino 35 na fimbo maalumu kwa watu wenye matatizo ya kuona 35.

“ASA mmekuwa mkitoa misaada mbalimbali kwa ajili ya watu wenyeulemavu na tumekuwa tukitumia nafasi hii kuwaomba wadau wengine kuiga mfano wenu pia mmeendelea kushirikiana na serikali kutoa huduma kwa watu wenye mahitaji maalumu si jambo dogo kwa leo tutapokea viti mwendo pisi 35 mafuta kwa ajili ya watu wenye ualubino 35 na fimbo maalumu 35,”alisema

Profesa Katundu alisema serikali inaendelea kuhamasisha taasisi nyingine kuiga mfano katika kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu ili kuimarisha maendeleo yao, ustawi na taifa kwa ujumla.

Kwa Upande wake Mwanasheria wa Taasisi ya ASA microfinance Zephania Paul alisema vifaa vilivyotolewa na asasi hiyo vinathamani ya Tsh. Milioni 13.5 huku akisisitiza kuwa lengo ni kuona umuhimu wa kuishi na watu wenye mahitaji maalumu kwa kichache kinachopatikana.

“Taasisi yetu ya ASA imekuwa ikifanya hivy mara kwa mara kwa lengo la kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha anawaboreshea maisha Watu wenye Ulemavu nchini,”alisema

Katibu Mkuu,Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Prof. Jamal Adam Katundu (kulia) akikabidhi mafuta maalumu kwa ajili ya watu wenye ualbino kwa Mwenyekiti wa Shirika la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Mkoa Wa Dodoma Omary Lubuva (katikati) wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu iliyofanyika jijini Dodoma.

Akizungumza awali, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye ulemavu Mkoa wa Dodoma, Omary Lubuva amempongeza Mhe. Rais, Samia Suluhu Hassan kwa hatua mbalimbali anazochukua katika kutatua changamoto zao na kuhakikisha wanashirikishwa katika shughuli mbalimbali za kukuza uchumi.

Ameongeza kuwa msaada huo waliopata ni muhimu kwani utawawezesha watu wenye ulemavu kujimudu na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali.

“Sisi Watu wenye Ulemavu tunatambua na kuthamini jitihada na juhudu zinazofanywa na serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia katika kutatua changamoto zetu, tunaomba taasisi na asasi nyingine waweze kuona haya ambayo yanafanywa na baadhi ya wenzao ili na wao waone wanawezaje kushiriki katika kusaidia kuboresha masha yetu,” alisema

Katibu Mkuu,Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu (katikati) akiwa pamoja na viongozi wengine wakimkabidhi kiti mwendo (wheelchair) Bi. Sofia Muhando wakati wa hafla hiyo.

Naye, Bi. Sophia Mhando (mwenye ulemavu wa Miguu) amesema hajawahi kufikiri kuwa ipo siku atapata kiti mwendo kwa kuwa amekuwa akihangaika kutembea na kuomba omba hivyo kupata kiti mwendo hicho kitamwezesha kujishughulisha na shughuli za ujasiriamali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *