UCHUKUZI SHWARI, WIZARA YA ARDHI MAMBO MAGUMU

Timu ya Mpira wa Miguu ya Uchukuzi imefanikiwa kuibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali SHIMIWI. mchezo huo

Mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Galanos, Jijini Tanga ulionekana kuwa na upinzani mkali kutoka kwa wapinzani wao, UCHUKUZI walionekana kucheza soka safi na lenye kuvutia lililowawezesha kupata ushindi wa Bao Moja lililofungwa na Mshambuliaji wao Stephano Meta, katika dakika ya 48 ya mchezo.

Washangiliaji wa timu ya Sekta ya Uchukuzi wakifurahia mara baada ya timu yao kuibuka kidedea dhidi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa bao 1-0, mchezo uliochezwa katika viwanja vya Shule ya Sekondari Galanosi, Jijini Tanga.

Aidha, katika mashindano hayo Uchukuzi Sports Club imeibuka na ushindi kwenye michezo mbalimbali ikiwemo mchezo wa Kuvuta Kamba ambapo waliibuka na ushindi wa mivuto 2-0 dhidi ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Kadhalika, upande wa mchezo wa Netiboli UCHUKUZI iliibuka na ushindi  wa magoli 38-5 dhidi ya TARURA kwenye mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Chumbageni Polisi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Bw. Mbura Tenga amesema wanaendelea kujifua kwa nguvu ili kufanikisha kutwaa Ubingwa wa Jumla wa mashindano hayo.

Timu ya Sekta ya Uchukuzi, wakipambana vikali dhidi ya timu ya Ardhi, katika mashindano ya Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Jijini Tanga

“Tuna uhakika wa kuendelea kufanya vizuri kwani timu zetu zimeanza vizuri tangu mashindano haya yalipoanza, tumepoteza mchezo mmoja tu upande wa mpira miguu lakini tunashukuru nao wamepambana leo tumeshinda mchezo huu wa pili. Hivyo tunaamini tutaendelea kufanya vizuri.” amesema Bw. Tenga.

Michuano Ya SHIMIWI inatarajiwa kufikia tamati Oktoba 15 ambapo washindi watazawadiwa zawadi mbalimbali vikiwemo vikombe na medali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *