WAKULIMA WA CHIKUYU-MANYONI WAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA MIRADI YA UMWAGILIAJI

Wakulima wa maeneo ya Chikuyu,Maweni na Kintinku wilayani Manyoni,Singida wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan na serikali ya awamu ya sita kupitia wizara ya kilimo kwa mikakati ya ujenzi wa miradi mipya ya umwagiliaji na ukarabati wa miradi ya zamani katika wilaya ya Manyoni.

“Mhe. Rais Samia anayo dhamira kubwa ya kumuona mkulima wa Tanzania ananufaika na kilimo chake kwa kulima kwa tija na kuongeza kipato kupitia kilimo cha uhakika cha umwagiliaji” Amesema Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde akiwa ziarani Manyoni, Singida.

Ameongeza kuwa Mhe. Rais ameelekeza eneo la Mbwasa,Manyoni kujengwa bwawa lenye thamani ya Tsh 20bn lenye uwezo wa uhifadhi maji wa mita za ujazo milioni kumi pamoja na skimu za umwagiliaji katika eneo hilo.

Aidha Naibu Waziri Mavunde,amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kusimamia ukarabati wa kingo za mto za mradi wa umwagiliaji Chikuyu sambamba na kufanya usanifu wa miradi ya Ntambaliza,Udimaa na Ngaiti ili kuwa na chanzo cha uhakika cha maji na miundombinu ya mifereji ya maji ya umwagiliaji

Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo yaliyojitokeza,Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa amesema kwamba Tume imejipanga kuhakikisha miradi yote mipya ya skimu za umwagiliaji inakuwa na chanzo cha uhakika cha maji ili kuruhusu shughuli za kilimo cha umwagiliaji kufanyika zaidi ya mara moja kwa mwaka.

Naye Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki Mhe. Dr. Pius Chaya kwa niaba ya wakulima wote amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kupitia wizara ya kilimo kwa kazi kubwa ya miradi ya umwagiliaji inayofanyika katika Wilaya ya Manyoni ambapo kupitia miradi hiyo wananchi wa maeneo hayo watakuza vipato vyao na kutatua changamoto kubwa ya Ajira hususani kwa vijana.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba ambaye anakaimu wilaya ya Manyoni kwa sasa Mhe. Suleiman Mwenda ameahidi kwa niabaya serikali ya wilaya kusimamia utekelezaji wa miradi hii kwa uadilifu na umakini mkubwa ili ilete matokeo chanya kwa wakulima wa mpunga wa skimu hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *