RAIS SAMIA SULUHU HASSAN KUFUNGUA MKUTANO WA 65 WA UNWTO.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika (65th UNWTO-CAF Meeting) utakaoanza tarehe 5 Oktoba 2022 katika ukumbi wa Hoteli ya Gran Melia jijini Arusha.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Arusha.

Amefafanua kuwa lengo la mkutano huo ni kujadili kuhusu mustakabali wa ustawi wa maendeleo ya sekta ya utalii barani Afrika hasa baada ya athari za mlipuko wa janga la UVIKO-19 iliyokuwa imeathiri utalii wa kimataifa kwa wastani wa kati ya asilimia 50 hadi 85 katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

Aidha, amesema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa ni mojawapo ya jitihada za Serikali katika kuongeza idadi ya watalii na kutanua wigo wa mazao ya utalii nchini kupitia uendelezaji wa mazao ya utalii ya kimkakati hususan Utalii wa Mikutano na Matukio.

Vilevile, ameweka bayana kuwa mkutano huo utawezesha kujengea uwezo wataalam na wadau wa utalii katika kutangaza utalii, kuendeleza na kufungamanisha mazao ya utalii katika kanda mbalimbali za utalii nchini kulingana na shabaha ya kuongeza idadi ya watalii kufikia watalii milioni 5 na mapato ya Dola za Marekani Bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.

“Mkutano huo ni nyenzo mojawapo ya kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais katika kutangaza utalii ndani na nje ya nchi kupitia programu ya Tanzania – The Royal Tour” Mhe. Balozi Chana amesema.

Mkutano huo wenye Kauli Mbiu ya “Kuujenga upya Utalii Stahimilivu wa Afrika kwa Maendeleo Jumuishi ya Kiuchumi na Kijamii” utahudhuriwa na Katibu Mkuu wa Shirika hilo Bw. Zurab Pololikashvili na kukutanisha mawaziri wenye dhamana ya masuala ya utalii na maliasili kutoka nchi wanachama wa UNWTO wa Kanda ya Afrika zaidi ya 50 na wadau wengine wakiwemo wataalam wa utalii na ukarimu katika ngazi ya kimataifa na kikanda, watoa huduma mbalimbali katika mnyororo wa utalii, wawekezaji, pamoja na watu mashuhuri zaidi ya 1.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *