
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Adolph Mkenda amempongeza Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh.Anthony Mavunde kwa ubunifu mkubwa na mipango mizuri katika kukuza sekta ya Elimu Jijini Dodoma.
Waziri Mkenda ameyasema hayo katika viwanja vya Chinangali,Jijini Dodoma wakati wa mashindano ya kusaka vipaji vya wanafunzi wa Shule za Msingi Jijini Dodoma ambapo jumla ya wanafunzi 600 walishindanishwa na wanafunzi 40 wakaibuka washindi na hivyo kupata fursa ya kufadhiliwa masomo kupitia shule ya Ellen White iliyopo Nzuguni,Jijini Dodoma.

“Nimefurahishwa sana na ubunifu mkubwa wa Mbunge wenu Mavunde kupitia uandaaji wa mashindano haya kusaka vipaji yaliyowashirikisha wanafunzi wa shule za msingi hapa Jijini Dodoma.
Ni wakati sasa wa kulea na kuendeleza vipaji vya wanafunzi katika mambo nje ya yale ya kitaaluma,ili kuwaandaa wanafunzi kuwa bora katika nyanja tofauti tofauti kama inavyofanyika hapa Dodoma Jiji.
Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mpango madhubuti ya kukuza elimu nchini na kuendeleza vipaji walivyonavyo wanafunzi na ndio maana tumekuja na mpango wa * Samia Scholarship* ambao ni ufadhili wa wanafunzi kwa ngazi ya Chuo Kikuu” Alisema Mkenda
Akitoa maelezo ya awali,Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde amesema msingi wa wazo hilo la uanzishwaji wa mashindano ya kusaka vipaji ni kuendeleza na kukuza vipaji vya wanafunzi Jijini Dodoma pasipo kuathiri uwezo wao wa kitaaluma.

Programu hii ilianza kwa ufadhili wa wanafunzi 20 kwa mwaka 2019/2020 na mwaka huu 2022 kufikia wanafunzi 40 wa darasa la V na VI ambao wanafunzi hao wote watagharamiwa ada kwa gharama ya Tsh 240m kwa miaka miwili.
Aidha Mhe. Mavunde pia ameeleza mpango wake wa kukuza elimu kupitia Habari,Mawasiliano na Teknolojia ambapo mpaka hivi sasa ameshagawa Vishkwambi (Tablets) kwa shule za msingi 20 vyenye thamani ya Tsh 3bn na kuendeleza zoezi la kugawa Computer kwa Shule zote 130 za Serikali za Msingi na Sekondari Jijini Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji,Afisa Elimu Msingi wa Jiji la Dodoma Bi. Prisca Myalla amempongeza Mbunge Mavunde kwa mchango mkubwa anaoutoa kwenye sekta ya elimu hasa uanzishwaji wa ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari na kuahidi kupitia serikali kuunga mkono jitihada za Mbunge Mavunde





