
TARURA imeendelea na mipango ya kuboresha Mtandao wa barabara za Wilaya kwa maeneo ambayo ni korofi vijijini na kuongeza ufanisi katika kusimamia menejimenti ya barabara za Wilaya ambazo zina mchango mkubwa kwenye shughuli za kiuchumi na kijamii na Mjini.
Hayo yamesema na Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor H. Seif katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika jijini Dodoma leo tarehe 03 Novemba 2022 uliokuwa na lengo la kueleza utekelezaji wan shughuli za Wakala Wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Mhandisi Seif amesema takwimu zinaonyesha asilimia 75.67 ya mtandao wa barabara za Wilaya ni za udongo na zinaathirika sana katika misimu ya mvua hali inayopelekea maeneo mengi kutofikika kwa urahisi na kwa kutambua hilo TARURA imejiwekea mipango mikakati ya muda mfupi na muda wa kati ili kutatua changamoto hizo.
“Kwa sasa TARURA inatekeleza Mpango Mkakati wake wa Pili wa miaka mitano ikiwa huu mwaka 2022/23 ni mwaka wa pili wa Mpango Mkakati wa pili, Mpango Mkakati wa kwanza wa TARURA ulianza kutekelezwa TARURA ilipoanzishwa tarehe 1 Julai 2017 na kukamilika tarehe 30 June 2021 ambapo jumla ya Shilingi 1,297.79 milioni fedha za ndani zilitumika.”
“Katika kipindi hicho jumla ya barabara zenye urefu wa kilometa 24,979.24 zilifanyiwa matengenezo, kilometa 955.35 zilijengwa kwa kiwango cha lami na kilometa 16,857.82 zilijengwa/karabatiwa kwa kiwango cha changarawe. Aidha, jumla ya madaraja 231 (kutoka Madaraja 2,960 hadi 3,191) na Makalvati 1,325 yamejengwa (kutoka Makalvati 67,992 hadi 69,317)”

Mhandisi huyo ametanabaisha mpango mkakati wa pili kutayarishwa kwa kuzingatia kuondoa vikwazo kwenye mtandao wa barabara za Wilaya ili ziwezekupitika misimu yote, kupandisha hadhi (upgrading) barabara za udongo kuwa za Changarawe(Lami).
“Mpango Mkakati wa pili umetayarishwa kwa kuzingatia vipaumbele vya, Kuzitunza Barabara zilizo katika Hali Nzuri na Hali ya Wastani kubaki katika hali hiyo ili kulinda uwekezaji ambao tayari umeshafanyika.
Kuondoa vikwazo kwenye mtandao wa barabara za Wilaya ili angalau ziweze kupitika misimu yote,
Matumizi ya tekinologia na malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi (mawe) katika ujenzi na matengenezo ya barabara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kutunza mazingira,”
“Kupandisha hadhi (upgrading) barabara za udongo kuwa za Changarawe/Lami kwa kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano wa magari katika majiji, manispaa na miji.”
“Hivyo kuanzia mwaka 2021/22 hadi 2026/27 lengo letu ni kuwa mtandao wa barabara za lami utaongezeka kwa km 1,450.75 (kilometa 2,404.90 – 3,855.65), changarawe km 73,241.57 (kilometa 29,116.57 – 102,358.14) na madaraja 3,808 (toka 2,812 hadi 6,620) ambapo fedha zitakazotumika kwenye mpango huu zinakadiriwa kuwa Zaidi ya Shilingi trilioni 4.2.”

Aidha amesema mkakati wao wa pili unalenga kufikia asilimia 85 ifikapo mwaka 2025/2026 ya barabara za Wilaya huku mpango huo ukiakisi kauli mbiu ya “TARURA TUNAKUFUNGULIA BARABARA KUFIKA KUSIKOFIKIKA”
“Lengo la Mpango Mkakati wetu wa pili ni kuwa ifikapo 2025/26 asilimia 85 ya mtandao wa barabara za Wilaya chini ya TARURA zitakuwa zinapitika kwa misimu yote na nyakati za mvua hapatakuwa na taharuki inayojitokeza sasa kwa maeneo mengi kutofikika,Katika Utekelezaji Mpango Mkakati wetu wa pili 2021-2026, Hadi kufikia Mwezi Juni 2022 jumla ya Shilingi bilion 673.3 zilipokelewa ikiwa ni asilimia 93 ya bajeti iliyotengwa na utekelezaji umefikia asilimia 81. Jumla ya km 22,202.84 zimefanyiwa matengenezo ya kawaida, km 275.85 zimejengwa kwa kiwango cha lami, km 11,120.09 zimejengwa kwa kiwango cha changarawe na jumla ya madaraja 596 yamejengwa/yamekarabatiwa.”

Ametanabaisha jumla ya Shilingi Bilioni 838.16 TARURA kutengewa ambapo kati ya Bizo Shilingi bilioni 776.63 ni fedha za ndani na Shilingi Bilioni 61.53 ni fedha za nje huku lengo la mwaka huu wa fedha 2022/2023 likiwa ni kufanya matengenezo ya kawaida km 21,595.72, kujenga/kukarabati km 422.07 kwa kiwango cha lami, kujenga/kukarabati km 11,074.56 kwa kiwango cha changarawe na kujenga/kukarabati madaraja 269 .
“Mwaka wa fedha 2022/23 ni mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa pili ambapo TARURA imetengewa bajeti ya jumla ya Shilingi bilioni 838.16 ambapo kati ya hizo Shilingi bilioni 776.63 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 61.53 ni fedha za nje. Katika utekelezaji wa bajeti ya Mwaka 2022/23 jumla ya zabuni 1,706 zenye thamani ya Shilingi bilioni 621.66 zimepangwa kutangazwa. Awamu ya kwanza tulitangaza asilimia 60 ya bajeti sawa na zabuni 1,085 zenye thamani ya Shilingi bilioni 378.56, ikiwa ni ununuzi wa asilimia 60 ya bajeti ili kazi zianze mapema kabla ya msimu wa mvua kuanza. Lakini pia, tumeanza utekelezaji wa awamu ya pili ya asilimia 40 iliyobaki. Katika awamu ya kwanza mikataba 969 imeshasainiwa na kazi zimeshaanza maeneo mbalimbali.”
“Zabuni 1,700 ambazo gharama ya kila zabuni ni chini ya Shilingi bilioni 3 zinatangazwa kwenye ngazi ya TARURA Mikoa na Zabuni 6 ambazo gharama yake ni Zaidi ya Shilingi bilioni 3 zinatangazwa katika ngazi ya TARURA Makao Makuu.”

Sanjari na hayo ameeleza uwepo wa Miradi Ya Maendeleo Inayogaramiwa Na Wadau wa Maendeleo ambayo ni Mradi ya Agriconnect (Jumuiya ya Ulaya), Roads to Inclusion and Socio-economic Opportunities (RISE),Ujenzi wa Daraja na Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi,Mradi wa Uendelezaji wa miji 45 (TACTIC) na Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam.
“Mradi wa Agri-connect awamu ya pili unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya ambapo jumla ya km 43.82 zitajengwa kwa kiwango cha lami (TZS 22.5 bilioni). Mradi huu unatekelezwa katika Wilaya za Kilolo km 1.1, Wanging’ombe km 19.3, Busokelo km 6.41, Mbozi km 11.01, na Rungwe km 6. Usanifu wa miradi hiyo umeshakamilika na sasa tupo kwenye hatua ya Ununuzi.”
“Mradi wa Barabara wa Kuongeza Fursa za Kiuchumi na Kijamii Nchini (RISE) ikiwa ni Mkopo nafuu toka Benki ya Dunia US $ 350 milioni. Mradi huu utajenga kilomita 535 za lami, (Km 400 za TARURA na Km 135 za TANROADS). Aidha, mradi utafanya matengenezo ya sehemu korofi Kilomita 2,900 na matengenezo ya kawaida Kilomita 23,000 katika Barabara za Wilaya chini ya TARURA, Mkataba wa Mkopo huu kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia ulisainiwa tarehe 19 Agosti 2021 na utekelezaji wa mkopo huo umeanza rasmi tarehe 16 Novemba 2021. Utekelezaji utaanza na ujenzi wa barabara za Wenda – Mgama km 19 na Mtilili – Ifwagi km 14 zilizopo kwenye Halmashauri za Wilaya ya Iringa na Mufindi mtawalia ambapo utekelezaji upo kwenye hatua za awali za manunuzi. Vilevile, usanifu wa barabara km 50 za mwanzo kwa kila Halmashauri utaanza kwa Halmashauri za Ruangwa, Mbogwe na Handeni.”
“Mradi wa ujenzi wa daraja na uendelezaji Bonde la Msimbazi Dar es Salaam (US $ 260 milioni). Mradi upo katika hatua za maandalizi ambapo usanifu wa Daraja la Jangwani umekamilika na maandalizi ya nyaraka muhimu za mambo ya kijamii na mazingira (Environmental and Social Safe guard Documents) yamekamilika. Upembuzi yakinifu pamoja na usanifu wa miundombinu ya mto (Down/up stream infrastructure umekamilika.
“Mkataba wa Mkopo (financing agreement) kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia umesainiwa tarehe 30 Septemba, 2022 na mradi unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 31 December, 2022. Taratibu za kuwapata wakandarasi wa ujenzi zitaanza mwezi Novemba 2022. Kazi za ujenzi za mradi huu zinatarajiwa kuanza ndani ya mwaka wa fedha 2022/23”
“Mradi wa Uendelezaji Miji 45 (TACTIC) (US $ 268 milioni) ikiwa ni mkopo nafuu toka Benki ya Dunia. Mradi uko kwenye hatua za mwisho za maandalizi ambapo usanifu wa miradi katika miji 12 ya mwanzo umekamilika. Mkataba wa mkopo kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia ulisainiwa tarehe 16 Juni, 2022 na mradi unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 14 Octoba, 2022. Taratibu za manunuzi ili kuwapata wakandarasi wa ujenzi pamoja na wataalamu washauri wa uasanifu wa miradi ya kundi la pili la miji 15 zitaanza mwezi Novemba, 2022. Kazi za ujenzi zinatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2022/23 na Mradi wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (DMDP) ikiwa ni mkopo nafuu toka Benki ya Dunia uko kwenye hatua yamatayarisho ikiwa ni pamoja na uibuaji wa mirafi.”

Amehitimisha kwa kusema kuwa kipaumbele chao ni kutumia malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi ili kupunguza garama za ujenzi na hadi sasa wamejenga madaraja 110 yenye thamani ya Shilingi Bilion 5 ambapo gharama imepungua kwa zaidi ya asilimia 50, ambapo Madaraja hayo yamejengwa katika mikoa ya Kigoma 72, Singida 13, Tabora 3, Kilimanjaro 6, Mbeya 2, Arusha 4, Mrorgoro 2 na Iringa 9, sambamba na kuendelea kufanya majaribio ya kiteknologia ili kutumia udongo uliopo eneo la kazi badala ya kusomba kutoka maeneo mengine ya mbali.