
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA ), Dkt. Stephan Ngailo amesema maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani kwa mwaka 2022 hapa nchini yatafanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia Oktoba 11 na kufikia kilele Oktoba 13 mwaka huu.
Dkt. Ngailo amebainisha hayo leo Oktoba 3,2022 Jijini Dar es Salaam akizungumza na Waandishi wa habari na ameeleza kilele chake kitakuwa katika viwanja vya Kimondo, Mlowo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoa wa Songwe.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Waziri wa Kilimo, Mh. Hussein Bashe, katika maadhsimisho hayo wataalam mbalimbali kutoka taasisi za utafiti, makampuni ya mbolea, vyuo vikuu, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa kilimo watapata fursa ya kutoa elimu kwa wakulima ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea, afya ya udongo, matumizi ya mbegu bora na udhibiti wa tasnia ya mbolea kwa ujumla,” amesema Dkt. Ngailo.
Ameeleza kwamba lengo la maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani ni kupania wigo zaidi wa kuelezea masuala mbalimbali katika tasnia ya mbolea ikiwemo mafanikio ya tasnia ya mbolea nchini, kutoa elimu ya kwa wadau wa mbolea hususan wakulima na wafanyabiashara wa mbolea.
“Siku ya Mbolea Duniani kwa mwaka 2022 ni “Ajenda 10/10: Matumizi Sahihi ya Mbolea ya Ruzuku kwa Kilimo chenye Tija”. Amesema kauli mbiu hiyo inalenga kuonesha juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuthamini mchango wa Sekta ya Kilimo ambapo katika msimu wa 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 150 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa utoaji Ruzuku ya Mbolea kwa wakulima ili kuwapunguzia makali ya bei mbolea.