Dodoma

Jeshi la Polisi Nchini limeanza kutekeleza maagizo mbalimbali yaliyotolewa na Mhe.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu
aliyoyatoa kwa nyakati tofauti kuhusiana na mafunzo kwa askari na Maafisa wa Jeshi la
Polisi ambapo Maaofisa Wakuu Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi pamoja na
maofisa wengine wa Jeshi hilo wameanza kupewa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea
uwezo.

Akifungua Warsha ya siku tano inayofanyika jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Christopher Kadio amesema kuwa, Jeshi la Polisi lijikite katika
kuboresha mkakati wa mawasiliano na kujenga taswira chanya kwa jamii.
Aidha, Katibu Mkuu, Christopher Kadio ametaja maeneo manne ya weledi ikiwemo
uwajibikaji, uhalali, ubunifu pamoja na mshikamano wa kitaifa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, kamishna wa Utawala na Menejimeti
ya Rasilimali Watu CP Benedict Wakulyamba amesema kuwa, Mkuu wa Jeshi la Polisi
ameanza kutekeleza maagizo hayo kwa kutumia miundombinu mbalimbali kwa lengo la
kutoa mafunzo ili kufikia malengo na matarajio ya serikali kwa kuanza na kundi la
kwanza la Warakibu Waandamizi wa Polisi ambao ni Wakuu wa Upelelezi Mikoa, Wakuu
wa Usalama Barabarani Mikoa na Wakuu wa Polisi Wilaya ambao hivi sasa wanapatiwa
mafunzo ya wiki sita katika Chuo cha Maafisa wa Polisi kilichopo Kidatu mkoani
Morogoro.

Naye msemaji wa IPRT (INSTITUTE OF PUBLIC RELATIONS IN TANZANIA) ambao ndiyo
wanaoendesha mafunzo hayo kwa kushirikiana na wadau wengine, Bwana William
Kallage amesema, taasisi hiyo imeanza awamu ya kwanza ya kutoa mafunzo ya
mawasiliano ya kimkakati na uongozi ili kuwajengea uwezo Maofisa wa Makao Makuu
ya Polisi na kisha baadae kuendelea na awamu nyingine kwa watendaji wa Jeshi hilo.



